![]() |
| Diwani wa kata ya Mlangarini akikagua barabara katika kitongoji Cha kiseriani |
Na Mwandishi wetu,Arusha
Wananchi wa Kitongoji cha Kiseriani, Kata ya Mlangarini, Wilaya ya Arusha, wamefanikiwa kukarabati barabara zilizokuwa zimeharibika kwa kiasi kikubwa, baada ya kuchangishana fedha pamoja na kutumia nguvu kazi yao.
Ukarabati huo umefanyika kwa ushirikiano wa wananchi na Diwani wa Kata ya Mlangarini, Bw. Emanuel Mrema, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha miundombinu katika eneo hilo.
Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hizo, Diwani Mrema alisema Kitongoji cha Kiseriani ni mfano wa kuigwa katika Kata ya Mlangarini na hata katika Halmashauri, kutokana na hatua wananchi walizochukua kuboresha miundombinu yao.
Mrema alisema hatua hiyo ni jambo zuri linalopaswa kuigwa na jamii nyingine, huku akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kusubiri bajeti kuu ya Serikali pekee ili kutatua changamoto za miundombinu katika maeneo yao.
“Wakati tunasubiri bajeti ya Serikali kuu, ni muhimu na sisi kama jamii tukajigusa kidogo, ili hata bajeti inapokuja itukute tukiwa tumeshapiga hatua kubwa, kwani barabara ni nguzo muhimu sana ya kuleta maendeleo,” alisema Mrema.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kutatua changamoto za msingi unaweza kusaidia kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma katika maeneo mbalimbali.

No comments:
Post a Comment