Na Mwandishi wetu,
maipacarusha20@gmail.com
Diwani wa Kata ya Mlangarini, Bw. Emanuel Mrema, amefungua semina kwa maafisa mikopo wa kata hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwaongezea ujuzi na kuwajengea uwezo wa kuwasaidia wananchi kupata na kutumia fursa za mikopo kwa maendeleo.
Semina hiyo imefanyika Agosti 16, 2026 katika Ofisi za Kata ya Mlangarini, ambapo Mrema amesema lengo kuu ni kuwapa maafisa hao uelewa na malengo ya kazi zao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mrema amesema moja ya majukumu muhimu ya maafisa mikopo ni kuleta mabadiliko katika jamii, hususan katika sekta ya ukopeshaji, akieleza kuwa Serikali imeendelea kuweka fedha kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupitia fursa mbalimbali za mikopo.
Amesema fursa za mikopo ni kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kuzitumia kwa kufuata kanuni, taratibu na masharti yaliyowekwa ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.
Amesema changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya wananchi katika kupata mikopo ya Serikali ni kutofahamu taratibu na masharti ya mikopo hiyo, hali ambayo imekuwa ikiwafanya wengi kushindwa kutumia
fursa hizo ipasavyo.
Kutokana na hali hiyo, Mrema amesema maafisa mikopo wameletwa katika Kata ya Mlangarini ili kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu fursa zilizopo, huku akisisitiza kuwa jukumu lao ni kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha, amesema matarajio yao ni kuona Kata ya Mlangarini ikiwa na vikundi vingi vya mikopo vinavyofanya shughuli za maendeleo na kutumia mikopo hiyo kwa tija, badala ya kuanzisha vikundi kwa ajili ya kupata fedha pekee.
Mrema amewataka maafisa mikopo kutowasubiri wananchi wafike ofisini, bali kuwafuata katika maeneo wanayoishi na kuwaelewesha umuhimu wa kutumia mikopo hiyo ambayo inalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo wamesema watatumia mafunzo hayo kuongeza ujuzi wao na kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi, huku wakiahidi kufanya kazi kwa lengo la kuhakikisha jamii inanufaika na fursa za mikopo zilizopo
Mwisho

No comments:
Post a Comment