Na Mwandishi wetu,Arusha
Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Tanzania - TAKUKURU Mkoa wa Arusha, imefanya warsha iliyojumuisha viongozi wasimamizi wa miradi ya maendeleo kisekta wa Taasisi za Umma za Mkoa huo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, leo Agosti 10,2026.
![]() |
Akisoma taarifa ya TAKUKURU mkoa, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngajilo amesema kuwa, warsha hiyo imelenga kujadili wajibu wa wadau katika usimamizi na utekelezaji wa Programu na Miradi ya Maendeleo, sambamba na kuweka mikakati madhubuti ya kutekeleza na kusimamia miradi katika mkoa huo.
Amebainisha kuwa, mkakati itakayowekwa kwenye warsha hiyo, itasaidia kutekeleza Programu na miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vigezo, ikiwemo miradi kutekelezwa na kukamilika kwa wakati, ubora unaendana na thamani ya fedha za Umma, ushiriki wa wadau kwenye utekelezaji wa miradi ikiwemo wananchi, ili kuboresha utoaji wa huduma pamoja na kuzuia watumishi kujihusisha na vitendo vya rushwa.
"Ninapenda kuwakumbusha wadau wote wenye dhamana ya usimamizi wa miradi ya maendeleo kwamba, tunao wajibu wa pamoja wa kusimamia utekelezaji wa miradi yote, na kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha, kufikia malengo yaliyokusudiwa, hii inatukumbusha kulinda rasilimali za Umma na kujiepusha na vitendo vya rushwa". Amefafanua Zawadi
Aidha, Zawadi ameweka wazi kuwa, warsha hiyo imekuja kufuatia mapungufu ambayo yamekuwa yakibainika wakati TAKUKURU inapofuatilia na kuchunguza usimamizi na hatua za utekelezaji wa programu za miradi ya maendeleo na kuzitaja changamoto hizo ni pamoja na viashiria vya uvujaji wa rasilimali, ucheleweshaji wa miradi, ushiriki mdogo wa wadau, hatari ya kutofikiwa kwa thamani halisi ya fedha, nia ovu za kujipatia maslahi binafsi zinazofanywa na baadhi ya wenye dhamana ya usimamizi wa miradi husika.
Awali, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita, chini Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa utashi na azma yake ya kutokomeza Rushwa Nchini, na kuiwezesha TAKUKURU kuimarisha Mapambano dhidi ya Rushwa nchini pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa chini ya Mhe.CPA Amos Gabriel Makalla kwa ushirikiano.



No comments:
Post a Comment