RC Sendiga ataka adhabu Kali wanaoingiza nchini Dawa bandia na duni - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 20 August 2026

RC Sendiga ataka adhabu Kali wanaoingiza nchini Dawa bandia na duni

 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga

 







Mussa Juma, Babati 


maipacarusha20@gmail.com 


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuendelea kutoa adhabu Kali kwa wanaoingiza nchini Dawa za Binadamu na mifugo  ambazo ni Bandia, Duni na hazijasaliwa na Mamlaka hiyo ili kukomesha Vitendo hivyo.

Sendiga amesema wanaoingiza nchini Dawa hizo na  wanaowasaidia wanakosa huruma na uzalendo kwa Taifa lao kutokana na madhara ya Dawa hizo.

Akifungua kikao Kazi cha siku mbili kati ya TMDA, wahariri na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Leo August 20,2026,Sendiga amesema suala la afya ni moja ya vipaumbele vya Serikali na limeainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.


Sendiga alipongeza jitihada za TMDA kuendelea  kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu majukumu ya TMDA, udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na changamoto zinazojitokeza katika eneo hilo.

Amesema taarifa sahihi kuhusu bidhaa za tiba ni muhimu kwa sababu sekta hiyo inahusisha moja kwa moja afya na mustakabali wa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili waweze kufanya maamuzi salama kuhusu matumizi ya dawa na vifaa tiba.

Sendiga amesema TMDA ina jukumu muhimu la kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyowafikia wananchi vinakuwa na ubora, usalama na ufanisi, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, hususan vyombo vya habari ambavyo vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii.

Mkuu huyo wa Mkoa hata hivyo alishauri tafiti zaidi juu ya matumizi ya Dawa za asili katika tiba mbalimbali.

"Dawa za asili zimekuwa na mchango mkubwa katika tiba ...na nchi nyingi wanatumia "amesema


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo wa TMDA, Dk. Yona  Mwalwisi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, inayoiwezesha kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.

Dk.Mwalwisi amesema TMDA imejenga utamaduni wa kukutana na wahariri na waandishi wa habari kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini ili kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuboresha udhibiti wa bidhaa za tiba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Amesema utafiti wa kuridhika kwa wananchi na wateja uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hususan Shule ya Biashara, mwezi Desemba 2022 katika halmashauri 35 za mikoa 16, umeonesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu TMDA kutoka asilimia 47 mwaka 2020, huku kiwango cha kuridhika na huduma za mamlaka hiyo kikiwa asilimia 82.

Dk.Mwalwisi amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano kati ya TMDA na vyombo vya habari, ambavyo vimekuwa daraja muhimu la kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba, pamoja na kuwaelimisha kuhusu hatari za bidhaa bandia, duni na zisizosajiliwa.


Amesema TMDA  imetambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa mamlaka iliyofikia ngazi ya tatu ya ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa bidhaa za tiba, huku ikiendelea na juhudi za kufikia ngazi ya nne, ambayo ndiyo ya juu zaidi, na kuendelea kuwa miongoni mwa mamlaka zinazoongoza barani Afrika.

Dk.Mwalwisi amesema mamlaka hiyo imeimarisha ufuatiliaji wa usalama wa dawa na chanjo baada ya kuingia sokoni, ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kufuatilia madhara ya dawa na chanjo hadi kufikia vituo 33 nchini, huku mtandao wa maabara hamishika ukiongezeka kutoka 19 hadi 28, hatua inayowezesha upimaji wa sampuli katika maeneo mbalimbali kwa wakati.


Dk. Mwalwisi amesema kikao hicho pia kinalenga kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, mikakati ya TMDA katika kupambana na bidhaa bandia, duni na zisizosajiliwa, pamoja na kuwafahamisha kuhusu fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa za tiba nchini ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.    

Akitoa mada katika kikao Kazi hicho,,Meneja kitengo cha sheria TMDA, Martha Malle amesema Mamlaka hiyo inakusudia kufanya maboresho ya Sheria ili kuongeza adhabu kwa wanaopatikana na Dawa bandia,duni na ambazo hazijasajiliwa na TMDA.

Hata hivyo Malle amesema Mamlaka hiyo Kwa kushirikiana na vyombo vingi  vya Dola vimeendelea kudhibiti Dawa bandia,duni na ambazo hazijasajiliwa na Mamlaka hiyo na watuhumiwa kadhaa wamekatwa na kufikishwa mahakamani.

Mwisho

No comments: