WAAJIRI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WAFANYAKAZI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 20 August 2026

WAAJIRI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WAFANYAKAZI


 




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com 


WAAJIRI wametakiwa kushirikiana na vyama na mashirikisho ya wafanyakazi ili kuboresha mahusiano kazini, kuongeza ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kigoma Malima, aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (DOWUTA).


Malima alisema vyama vya wafanyakazi vimebadilika na sasa vinadai haki za wafanyakazi huku vikihimiza wanachama wao kutimiza wajibu, hatua ambayo alisema inalenga kuleta usawa na tija mahali pa kazi.


“Ni lazima kuwepo ushirikiano kutoka kwa pande zote. Waajiri wawatuze vizuri wafanyakazi, na wafanyakazi nao watimize wajibu wao ili kupata matokeo mazuri,” alisema Malima.


Aliwataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri kuweka utaratibu mzuri wa mawasiliano kati yao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima na kujenga mazingira bora ya kazi.


Aidha, aliwataka viongozi wa DOWUTA kutokubali kutumiwa na wanaharakati au wanasiasa, bali kuzingatia maslahi ya wafanyakazi na wanachama waliowachagua.


Malima aliongeza kuwa katika bandari zote duniani ni lazima kuwepo makuli, bila kujali kiwango cha mitambo ya kisasa na teknolojia inayotumika, akisisitiza kuwa mchango wa nguvu kazi ya binadamu utaendelea kuwa muhimu.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DOWUTA, Mwalami Manyara, alisema jukumu la chama hicho ni kutetea haki za wafanyakazi na kulinda haki za waajiri.


“Huwezi kudai haki bila kutimiza wajibu. DOWUTA ina jukumu la kutetea haki za wafanyakazi, kulinda haki za waajiri na kuisaidia Serikali katika hatua za ukodishaji wa bandari zake,” alisema Manyara.


Mwisho.

No comments: