HALMASHAURI YA WILAYA YA KARATU YAJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA CSR TARIME - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 24 September 2026

HALMASHAURI YA WILAYA YA KARATU YAJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA CSR TARIME

 



Na Mwandishi wetu 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Ndg, Juma Hokororo pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara  wamefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kujifunza namna bora ya utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR).


Mafunzo hayo yaliongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Ndg. Solomon Shati, akishirikiana na wakuu wa idara ambapo Katika ziara hiyo, wamejifunza mifumo na taratibu zinazotumika Tarime kufanikisha miradi ya CSR.


Aidha Katika sekta ya afya, wametembelea Hospitali ya Halmashauri iliyopo Nyamwaga na kujionea miradi iliyokamilika, ikiwemo wodi ya watoto, jengo la madawa, na miundombinu ya njia za kupita wagonjwa.


Upande wa sekta ya elimu, walitembelea Shule ya Sekondari Matongo ambapo walishuhudia maabara za sayansi zilizokamilika, jengo la utawala, pamoja na nyumba mbili za walimu. 


Akizungumza wakati wa ziara hiyo na kutoa shukrani zake kwa uongozi wa Tarime, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu, Ndg. Juma Mussa Hokoro alisema:


“Tunashukuru sana viongozi na wataalamu wa Halmashauri ya Tarime kwa ustahimilivu na maandalizi mazuri, Tumejifunza mambo mengi na makubwa, hususani katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii, Uzoefu tulioupata hapa utakuwa chachu kubwa ya kuboresha miradi ya CSR kule kwetu Karatu kwa maendeleo ya wananchi wetu.”


Ziara hiyo ilihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kuendeleza ushirikiano na kubadilishana uzoefu wa kazi ili kuinua kiwango cha utoaji wa huduma kwa jamii katika halmashauri zote mbili.

No comments: