VURUGU ZA WAKULIMA NA WAFUGAJI KILOSA: WATU WAWILI WAFARIKI, ASKARI 3 WAJERUHIWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 24 September 2026

VURUGU ZA WAKULIMA NA WAFUGAJI KILOSA: WATU WAWILI WAFARIKI, ASKARI 3 WAJERUHIWA





Na Lilian Kasenene, Kilosa-Morogoro

maipacarusha20@gmail.com 


VURUGU zinazodaiwa kuhusishwa na mgogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, zimesababisha vifo vya watu wawili katika matukio tofauti, kujeruhiwa kwa askari watatu na kuharibiwa kwa mali za Jeshi la Polisi.


Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, tukio la kwanza lilitokea Septemba 23, 2026, majira ya saa 7 mchana katika Mashamba ya Bondeni, Kitongoji cha Legeza Mwendo, Kijiji na Kata ya Tindiga, Tarafa ya Masanze.


Katika tukio hilo, Festo Selias Chaula, maarufu kwa jina la Walter Mkulima, alijeruhiwa vibaya.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema Festo alikatwa kichwani kwa kitu chenye makali na kupigwa kwa vitu butu sehemu mbalimbali za mwili, na kupata majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Mashamba ya miwa

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya ufuatiliaji na kuwakamata Seletwi Samiji Mdamanya na Paulo Lukas Sumai, ambao wanadaiwa kuhusika na mauaji hayo.


Wawili hao wanadaiwa kuwa wafugaji na wakazi wa Kijiji cha Malangali, Kata ya Tindiga.


Hata hivyo, wakati askari wakiwasafirisha watuhumiwa kwenda Kituo cha Polisi Kilosa, kundi la watu linalodaiwa kuwa wakulima, likiwa na takribani watu 200, lilidaiwa kufunga barabara na kuwashambulia askari waliokuwa wakiwasindikiza watuhumiwa hao.


Kwa mujibu wa Kamanda Kantimbo, kundi hilo lilikuwa na silaha mbalimbali za jadi na lililenga kuwadhuru watuhumiwa hao ambao ni jamii ya wafugaji.


Askari Polisi walidaiwa kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao waliokuwa na visu, mapanga, mishale, mikuki, marungu na mawe.


Baada ya kundi hilo kutawanyika, Polisi walifanya ukaguzi na kumkuta mmoja wa wananchi, Kelvin Mhagama, mkulima na mkazi wa Kichangani, akiwa amejeruhiwa kwa kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake.


Kelvin alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu.


Kamanda Kantimbo amethibitisha kuwa, mbali na kifo hicho, askari watatu walijeruhiwa katika vurugu hizo baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi na wanaendelea na matibabu.


Vurugu hizo pia zilisababisha pikipiki ya Polisi yenye namba PT 3131, aina ya SANLG, kuteketea kwa moto, huku gari la Polisi lenye namba PT 5877, aina ya Toyota Hilux, likiharibiwa baada ya kupigwa kwa mawe.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka wakulima, wafugaji na wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kutumia njia rasmi za kisheria katika kushughulikia migogoro kati ya wakulima na wafugaji.


Polisi pia linaendelea na msako wa kuwakamata watu wote wanaodaiwa kuhusika na vurugu hizo na kujichukulia sheria 


Mwisho.

No comments: