Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Mwanamke kutoka Uganda, Susan Muwonge, anatarajiwa kuandika historia katika mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania, yatakayofanyika Oktoba 1 hadi 4, 2026, baada ya kujitosa kushiriki kama dereva katika mashindano hayo.
Muwonge anakuwa miongoni mwa wanawake wanaoshiriki mashindano ya mbio za magari barani Afrika, huku akiwa dereva rasmi wa gari aina ya Subaru Impreza, akisaidiwa na Musa Nsubuga kama dereva msaidizi (co-driver).
Mashindano hayo ya awamu ya nne na ya mwisho kwa mwaka 2026 yatafanyika katika Shamba la Miti la Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), eneo la Makundi, mkoani Morogoro.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, Msimamizi Mkuu wa mashindano, Dk. Mosi Makau, alisema ushiriki wa Muwonge unatarajiwa kuongeza mvuto wa mashindano hayo na kutoa hamasa kwa wanawake zaidi kushiriki katika mchezo wa mbio za magari.
“Mashindano haya yatahusisha magari nane. Kwa Tanzania madereva wawili tu ndio watashiriki, huku wengine wakitoka Kenya, Zambia, India na Uganda,” alisema Dk. Makau.
Alisema kinachowapa fahari ni ushiriki wa Muwonge kama dereva, akieleza kuwa wanawake waliowahi kushiriki katika mashindano hayo walikuwa wakifanya kazi ya udereva msaidizi, tofauti na safari hii ambapo Muwonge ataendesha gari mwenyewe.
Kwa mujibu wa Dk. Makau, mashindano hayo yatahusisha jumla ya magari 23, ambapo magari nane yatashindania ubingwa wa African Rally Championship, huku magari 15 yakishiriki National Rally Championship.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mkwawa Group of Companies, ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Richard Sinamtwa, alisema mashindano hayo ni hatua muhimu katika kukuza mchezo wa magari na kuwaunganisha wadau wa mchezo huo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Sinamtwa alisema kupitia mashindano hayo Tanzania itaendelea kunufaika katika kukuza utalii na uchumi wa jamii, ikizingatiwa kuwa mchezo huo unawakutanisha washiriki na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali.
“Kupitia mashindano haya tuweze kutunza taswira ya Tanzania, kupitia michezo tuendelee kuhamasisha utalii, uhifadhi pamoja na kuhakikisha tunasimamia maendeleo ya jamii zetu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Tanzania, Satinder Singh Bardi, aliwataka wakazi wa Morogoro na mashabiki wa mchezo huo kuzingatia usalama wao wakati wote wa mashindano.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kufuata maelekezo ya vyombo vya usalama na kukaa katika maeneo yaliyotengwa kwa watazamaji ili kuepusha ajali na madhara.
Aidha, aliwahakikishia mashabiki kuwa maandalizi ya usalama yamezingatiwa ili mashindano hayo yafanyike kwa utaratibu na usalama.
Mwisho.




No comments:
Post a Comment