Mwandishi Wetu, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
KATIBU wa Jumuiya ya Mabaharia Tanzania (Old Navy), Daniel Masele, amewataka Watanzania kuacha kuangalia hifadhi na vivutio vya utalii kama maeneo ya wageni pekee, akisema ziara yao katika Bonde la Ngorongoro imewapa fursa ya kujionea utajiri wa asili ambao Tanzania imejaaliwa.
Masele alisema mabaharia hao, ambao wamekuwa wakisafiri katika maeneo mbalimbali duniani, wamekutana na mambo mengi katika safari zao, lakini baadhi ya yale waliyoyaona Tanzania ni ya kipekee na hawajawahi kuyashuhudia katika maeneo mengine waliyofika.
Alisema wakiwa Ngorongoro walishuhudia wanyama mbalimbali wanaoishi ndani ya Kreta ya Ngorongoro, jambo alilolitaja kuwa miongoni mwa maajabu yanayopaswa kuwafanya Watanzania kuwa wa kwanza kutembelea na kuitangaza nchi yao.
![]() |
Kwa mujibu wa Masele, Tanzania imekuwa ikipata mapato kupitia sekta ya utalii, huku sehemu kubwa ya wageni wanaotembelea vivutio hivyo wakitoka nje ya nchi. Hivyo, amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kuvifahamu vivutio vyao na kuwa mabalozi wa utalii wanapokwenda katika maeneo mbalimbali duniani.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mohamed Said Ngamba, ambaye alisema wazo la kuanzisha Old Navy lilitokana pia na kutambua nafasi waliyonayo mabaharia katika kuitangaza Tanzania kutokana na mazingira yao ya kazi yanayowapeleka katika nchi na maeneo mbalimbali duniani.
![]() |
Ngamba alisema wakiwa safarini baharini walikuwa wakifuatilia juhudi mbalimbali za kuitangaza Tanzania, ikiwemo kupitia filamu ya Royal Tour, na kuona kuwa nao wana wajibu wa kushiriki kuitangaza nchi yao kwa kuwaeleza watu wanaokutana nao kuhusu vivutio vilivyopo Tanzania.
Alisema mabaharia ni miongoni mwa wawakilishi wa Tanzania wanaokutana na watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo jumuiya hiyo imeamua kutumia nafasi hiyo kuhamasisha utalii kwa kutoa ushuhuda wa maeneo wanayoyatembelea wenyewe.
“Hatupaswi kukaa kimya wakati nchi yetu ina vivutio vingi. Kama tunasafiri na kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, tunapaswa kuwaambia Tanzania ina nini na kuwaalika waje kuona wenyewe,” amesema Ngamba.
Ameeleza kuwa ziara ya Ngorongoro ni sehemu ya mpango wao wa kutembelea vivutio mbalimbali nchini, wakianza na Mikumi na baadaye kutembelea maeneo mengine, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, ili wanapozungumza kuhusu utalii wa Tanzania wawe wameviona vivutio hivyo kwa macho yao.
Ngamba alisema katika ziara hiyo amevutiwa na mandhari ya Ngorongoro pamoja na wanyama mbalimbali aliowaona, akiwemo simba, faru, pundamilia na kiboko, akisema uzoefu huo utawapa nguvu zaidi katika kuwahamasisha wengine kutembelea Tanzania.
Mabaharia wengine walioshiriki ziara hiyo, Omary Said Kipelele, Siwatu Hassan Sembi, Fahad Mohamed na Miraji Omary, wamesema watatumia fursa walizonazo kuwahamasisha ndugu, marafiki na watu wanaokutana nao nje ya Tanzania kutembelea nchi hiyo na kushuhudia vivutio vilivyopo.
Walisema wanatambua umuhimu wa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza sekta ya utalii, huku wakimshukuru Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, kwa kusaidia kuwezesha safari zao za kutembelea hifadhi za taifa ili kupata uzoefu wa moja kwa moja wa vivutio wanavyotaka kuvitangaza.
Kwa upande wake, mdau wa utalii kutoka Kampuni ya Utalii ya Mbapari, Isaya John, alisema Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kutembelea hifadhi kwa kuwa gharama za kuingia kwa raia wa Tanzania zimewekwa katika viwango vinavyoweza kumudu.
Alisema wananchi hawapaswi kuziacha fursa hizo na kuwaachia wageni pekee, bali wanapaswa kutembelea vivutio vya ndani na kuvifahamu ili wawe mabalozi wazuri wa utalii wa Tanzania.
Wito huo umejitokeza pia wakati zaidi ya watu 1,700 waliokuwa wakishiriki Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL Week 2026), iliyofanyika Ngurdoto Mountain Lodge, Arusha, walipopata fursa ya kutembelea Ngorongoro na vivutio vingine jijini humo.
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Yasin Msangi, alisema washiriki hao walikutana Arusha kwa ajili ya wiki hiyo iliyofanyika Septemba 22 hadi 26, 2026.
Alisema zaidi ya washiriki 1,000 wakiwa na magari zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali za Afrika waliamua kutumia fursa hiyo kutembelea Ngorongoro na kujionea vivutio vilivyopo.
Msangi alisema ziara hiyo imewapa washiriki fursa ya kuona kwa vitendo kile ambacho mara nyingi hukisikia au kukisoma, huku akiwataka Watanzania wengine kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi na vivutio vya ndani.
Kwa upande wao, mabaharia hao walisema safari yao haitakuwa ya mara moja, bali wanatarajia kuendelea kutembelea maeneo mengine ya utalii nchini na kutumia uzoefu huo kuwaeleza wengine, hasa wanaokutana nao katika safari zao za kimataifa, kuhusu uzuri na utajiri wa Tanzania.
Mwisho




No comments:
Post a Comment