Mwandishi wetu, Geita
maipacarusha20@gmail.com
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt Steven Lemomo Kiruswa ameipongeza Equity bank kwa kuwajali wachimbaji madini na kuwapatia vifaa na mitambo ya uchimbaji.
Dkt Kiruswa ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea banda la EQUITY Bank kwenye maonyesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan manispaa ya Geita.
Amesema kupitia benki hiyo wachimbaji madini watanufaika kwa ufadhili wa vifaa na mitambo ya kuchimbia madini.
"Nimesikia mnatoa ufadhili wa vifaa vya mitambo kwa Excavator, Crusher, malori ya kubebea mchanga na Drilling Rigs, hongereni sana kwani mnawajali wachimbaji madini," amesema Dkt Kiruswa.
Mkuu wa idara ya wateja wa kati, rejareja na binafsi wa EQUITY Bank Tanzania Theresia Mayanie amewaasa wachimbaji madini waimarishe migodi yao kwa kumiliki vifaa vyao.
Mayanie amesema kupitia benki hiyo, wachimbaji wanaweza kupata vifaa na mitambo bila kulipa gharama zote kwa mara moja.
Ametaja baadhi ya vigezo vya kustahili ni watu binafsi na biashara wanaohitaji vifaa, magari na mitambo na uwezo wa kurejesha mikopo.
"Akaunti hai ya EQUITY Bank kwa angalau miezi mitatu, taarifa za benki za miezi 12 pale zinazohitajika na taarifa za fedha zilizokaguliwa za miaka mitatu pale zinazohitajika," amesema Mayanie.
Amesema faida ni kupata mtaji wa kusaidia shughuli za biashara, kuendelea bila kukwama, gharama, mahitaji muhimu ya uendeshaji na kuboresha mtiririko wa fedha.
Ametaja faida nyingine ni muda wa marejesho hadi miezi 36 kulingana na madhumuni ya mkopo, ufadhili unaozingatia mahitaji ya biashara na uwezo wa kifedha.
"Endesha mgodi wako bila kusimama, tunakuwezesha kwa mtaji wa uendeshaji kwa mafuta, baruti, mishahara, Reagents na vipuri," amesema.
MWISHO

No comments:
Post a Comment