Waandishi ibueni mapungufu kabla ya El-Nino kufika - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 27 September 2026

Waandishi ibueni mapungufu kabla ya El-Nino kufika

 




 

 

Mwandishi wetu, Dodoma 


maipacarusha20@gmail.com 


Waandishi wa habari za mazingira nchini, wameshauriwa kuandika sasa mambo yatakayoleta athari kutokana na Mvua za El- Nino ili kupunguza madhara  yanayoweza kuja kutokea.


Serikali imetangaza kuanzia mwezi ujao kuna uwezekano wa kunyesha mvua kubwa kupita kiasi za El Nino katika maeneo mengi nchini na hivyo kuleta madhara.


Akifunga mafunzo ya waandishi wa habari za mazingira kutoka mikoa ya Kanda ya Kati, yaliyoandaliwa na Taasisi ya wanahabari ya usaidizi wa Jamii za pembezoni (MAIPAC) kwa ushirikiano na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ( THRDC) Kwa udhamini wa shirika la umoja wa Mataifa la UNESCO, Mkurugenzi wa (MAIPAC), Mussa Juma amesema waandishi  wanapaswa kuibua mapungufu kabla ya El-Nino.


Juma anasema, bado kuna mapungufu  katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na athari za El- Nino hivyo badala kuendelea kuandika matamko ya viongozi pekee waandishi waibuwe mambo yanayopaswa kufanywa sasa.


"Kuna maeneo katika miji yetu bado mitaro imeziba, kuna maeneo vimetolewa vibali kujengwa nyumba au maeneo ya biashara kwenye njia za maji tuandike sasa ili Serikali na wadau wengine wachukuwe hatua" amesema Juma


Mkurugenzi huyo amesema, pia kuna ujenzi unaendelea wa barabara na miradi mengine na maji bado yameelekezwa kwenye makazi ya watu tuandike sasa wakandarasi waboreshe mifumo ya maji badala ya kusubiri maafa"anasema 


 Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa WA chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari (JOWUTA)  aliwaomba pia wanahabari kuandika habari za uchunguzi kwa nini sasa imeibuka tena migogoro ya wakulima, wafugaji na wahifadhi na kuanza kusababisha vifo.


 Naye Mkurugenzi wa miradi na uendeshaji wa THRDC ,Wakili Halima Sonda aliwataka waandishi waliopata mafunzo hayo Kuonesha tofauti katika uandishi wao.


"Nendeni mkaandike habari za mazingira ambazo zitachochea mabadiliko ya Sheria, sera, mitazamo na uwajibikaji" alisema Wakili Sonda


Wakili Sonda pia aliwataka wanahabari hao, kuzingatia Sheria na maadili ya uandishi wakati wakitekeleza majukumu yao.


Mafunzo hayo  yalishirikisha waandishi 35  kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya, Iringa, na Singida na tayari kwa waandishi mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Ziwa yamefanyika pia yatafanyika kwa  Dar es Salaam, Pwani,Tanga na Zanzibar.

mwisho

No comments: