![]() |
| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Andrew Kantimbo akikagua nyumba ambayo mtuhumiwa alijificha baada ya kuwaona polisi |
Na Lilian Kasenene, Kilosa-Morogoro
Maipacarusha20@gmail.com
TUKIO la kutekwa kwa mwanamke na mtoto wake katika Kijiji cha Parakuyo, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, limeishia kwa kifo cha Kokan State (30), baada ya kupigwa risasi na polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, Kokan alikuwa akitafutwa kwa tuhuma zinazohusisha mauaji, ubakaji na wizi wa kutumia silaha.
Kantimbo amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu.
Baada ya kubaini alipo na kufika eneo hilo, Kokan alimshika mwanamke aliyekuwa akimhudumia kinywaji pamoja na mtoto wake mdogo na kujifungia nao ndani ya chumba, akiwatumia kama kinga dhidi ya polisi.
Amesema Kokan alitishia kumuua mwanamke huyo na mtoto wake kwa kutumia sime iwapo polisi wangejaribu kumkamata.
Kutokana na hali hiyo, polisi walitumia silaha baada ya jitihada zote za kumshawishi mtuhumiwa ajisalimishe kushindikana, na kusababisha kifo chake.
Mwanamke aliyetekwa, Rehema Masuke, mkazi wa Kijiji cha Parakuyo, amesema tukio hilo liliwapa hofu kubwa, wakihofia kuuawa kwa kutumia sime aliyokuwa nayo kijana huyo.
Kwa upande wake, baba mzazi wa Kokan amesema kwa muda mrefu alikuwa akimkanya mwanawe kuacha kujihusisha na matukio ya uhalifu, lakini licha ya ushauri huo, kijana huyo alihusishwa mara kadhaa na matukio hayo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Parakuyo, Emmanuel Kibasisi, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama na kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na uhalifu.
Polisi mkoani Morogoro wameendelea kutoa wito kwa vijana kujiepusha na uhalifu na kutafuta kipato kupitia shughuli halali.
MWISHO.


No comments:
Post a Comment