Burhani Yakub,Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema halitarajii mabadiliko ya tabianchi yajayo ikiwamo mvua kubwa za el-nino kuharibu miundombinu yake kwa kuwa imejengwa kukabiliana na tahadhari hizo.
Mhandisi Mwandamizi wa TPDC upande wa kampuni tanzu ya maendeleo ya gesi (GASCO), Hassan Temba amesema hayo leo alipotakiwa na wanahabari kueleza Shirika hilo limejiaandaaje na mvua za El nino.
Amesema TPDC inaendesha miradi nchini ya kusimamia na kufanya shughuli za kitafiti na kuendeleza nishati ya gesi na mafuta kupitia kampuni zake tanzu za Gasco na Tanoil.
Amesema kupitia kampuni hizo inaendesha mitambo mikubwa ya kitafiti na kuchimba gesi katika miradi minne ya Mnazibay,Songosongo magharibi,Eyas Wembere na vitalu.
Amesema katika mitambo hiyo imejengwa kwa tahadhari kubwa ya endapo yatatokea mafuriko ili kuepuka kukosekana kwa umeme nchini.
"Mfano katika mafuriko yaliyopita mitambo ya kampuni nyingine ilizima baada ya kuzamishwa na kuingia maji lakini nchi haikukumbwa na uhaba wa umeme kwa sababu mitambo ya TPDC ya gesi ya kusukuma na kusambaza umeme haikuathirika"amesema Temba.
Mtaalamu huyo amesema tukio la kutoathirika kwa mitambo ya TPDC lilitokana na namna wahandisi walivyoijenga kwa kuzingatia tahadhari za kutokea mafuriko jambo lililozilazimu kampuni nyingine za ndani na nje ya nchi kwenda kujifunza namna ya kupambana na majanga
Afisa Uhusiano wa TPDC,Francis Lupokela amesema shirika hilo lilianzishwa rasmi mwaka 1969 na kuanza majukumu yake mwaka 1973 kwa kuendesha shughuli zake za utafiti na kuendeleza nishati ya gesi na mafuta.
"TPDC kupitia makampuni yake tanzu inatekeleza majukumu yake ya kila siku kitafiti na kuendeleza nishati kwa mkondo wa chini,Kati na juu....lakini pia inajenga matanki ya maghala mkakati kwa ajili ya kuhifadhi nishati ya akiba"amesema Francis.
Akizungumzia kuhusu mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki la Uganda hadi Tanga, amesema ni wa kimkakati unaohusisha ujenzi na uendeshaji wa mfumo wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Jijini Tanga.
Kwa upande wa Tanzania, amesema bomba hili linapita katika mikoa nane ambayo ni Kagera, Geita, Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, likiwa na urefu wa kilometa 1,147 ndani ya Tanzania.
Kwa Mkoa wa Tanga, mradi unahusisha sehemu yenye urefu wa kilometa 205.91, inayopita katika Wilaya za Kilindi, Handeni, Korogwe, Muheza, Mkinga na Jiji la Tanga.
"Hii ina maana kwamba Mkoa wa Tanga siyo tu eneo la mwisho la bomba hili, bali ni sehemu muhimu sana katika mnyororo mzima wa mradi wa EACOP.Chongoleani, Tanga, inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kupokelea na kusafirisha mafuta ghafi kwenda katika masoko ya kimataifa" amesema Francis
Amesema mradi huu unaongeza umuhimu wa Tanga kama eneo muhimu katika ramani ya shughuli za nishati na biashara za kimataifa.
Amesema wananchi wanaoguswa na miradi hiyo jumla yao ni 9,927 katika mikoa yote inapopita kati yao, 9,880 walikuwa wamesaini mikataba ya fidia na kupokea malipo ya fidia ya fedha taslimu yenye jumla ya Sh 35.078.BIlioni
Kwa Mkoa wa Tanga idadi ya waguswa ni 1,700, ambapo 1,689 wamekwishasaini mikataba ya fidia na fedha taslimu iliyolipwa kama fidia ni zaidi ya sh 10.495.biliini huku eneo la ardhi lililotwaliwa likiwa ekari 1,761.101
MWISHO

No comments:
Post a Comment