Uchaguzi viongozi wapya Burunge WMA waanza. Spika ajiondoa - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 13 September 2026

Uchaguzi viongozi wapya Burunge WMA waanza. Spika ajiondoa

 


Mwandishi wetu, Babati


maipacarusha20@gmail.com 


Halmashauri ya Babati vijijini, imetangaza kuanza  kwa uchaguzi wa viongozi wapya katika eneo la Hifadhi ya  Jamii ya  Wanyamapori ya Burunge, baada ya kukamilika maboresho ya Katiba ili kuifanya hifadhi hiyo kuwa bora barani Afrika.


Burunge WMA ipo katikati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara, mkoa wa Manyara  chini ya usimamizi wa halmashauri ya babati na Mamlaka ya usimamizi wanyamapori ( TAWA).       

Uchaguzi huo unafanyika baada ya kusimamishwa viongozi waliokuwepo madarakani kwa tuhuma kadhaa na baadae kumaliza muda wao.


Akizungumza na waandishi wa habari za Utalii na Uhifadhi wilayani Babati, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Babati vijijini, Anna Mbogo  jana anasema, uchaguzi  na maboresho hayo yanafanyika pia kwendana na dhamira ya Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kuongeza mapato ya Taifa kupitia Utalii.


Mbogo anasema tayari  maboresho ya Katiba na mfumo wa uendeshaji Burunge WMA umekamilika na sasa chaguzi  za viongozi wa jumuiya hiyo, zimeanza katika vijiji 10 vinavyounda jumuiya hiyo.


Anasema vijiji hivyo ni, Mwada Sangaiwe, Vilima Vitatu, Ngoley, Kakoi, Olasiti, Manyara, Magara, Maweni na Minjingu.


"Chaguzi zimeanza tunatarajia zikikamilika tutapa viongozi bora ambao wataweza kuja kusimama Uhifadhi, Utalii na kubwa kuongeza mapato ya Utalii kwa manufaa ya vijiji na serikali kwa ujumla"anasema


Anasema Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Dkt Samia Suluhu Hassan, tayari ilikamilisha kazi ya kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour hivyo, sasa kazi iliyopo ni kuweka mazingira mazuri ya kuvutia watalii katika maene yote yaliyohifadhiwa.


Mkurugenzi huyo anasema, katika eneo la Burunge WMA tayari matunda ya uhifadhi yameanza kuonekana baada ya hivi karibuni, hoteli ya Chem chem iliyopo  ndani ya hifadhi hiyo, kushinda tuzo ya Safari Luxury lodge Afrika na Tanzania tuzo zilizotolewa na shirika la Utalii duniani la WTA.


"Tuzo hii inaendelea kuitangaza Burunge WMA vizuri na itavutia watalii zaidi na tunaomba na wawekezaji wengine katika eneo hili kuboresha huduma zao ili kuendelea kuvutia watalii"anasema.  


Mbogo amewataka wananchi wenye sifa na nia ya dhati kuendeleza uhifadhi na Utalii katika vijiji hivyo kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali.




Spika wa Burunge WMA, Erick Lilayoni ambaye anamaliza muda wake, anasema mapato ya Burunge WMA yamekuwa yakiongezeka hadi kufikia takriban billion 4 kwa mwaka na vijiji vimekuwa vikipata mgao zaidi ya millioni 200 kwa mwaka.


"Binafsi sitarajii kugombea tena uongozi lakini naamini eneo hili tukilitunza vizuri, manufaa makubwa yataendelea kupatikana kwa wananchi wa vijiji 10 na serikali kwa ujumla"anasema.    


Baada ya kukamilika uchaguzi wa wajumbe wa WMA ngazi za vijiji baadae watachaguliwa viongozi wa kuongoza WMA.


MWISHO.

No comments: