![]() |
| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, |
![]() |
Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
KUNDI la ng’ombe linalodaiwa kuingizwa katika mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Mvomero, limeibua vurugu baada ya walinzi wawili wa kiwanda hicho kushambuliwa na kujeruhiwa wakati wakijaribu kuwaondoa mifugo hiyo katika mashamba.
Tukio hilo limetokea Septemba 23, 2026, saa sita mchana katika eneo la D6, ndani ya mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, alisema walinzi hao walifanikiwa kulikamata kundi la ng’ombe na kuanza kuwaswaga kuelekea Kambi ya Dumila One, inayomilikiwa na kiwanda hicho, kwa ajili ya utambuzi na hatua zaidi.
Aidha, alisema zoezi hilo lilikumbana na upinzani kutoka kwa wafugaji waliodaiwa kuwazuia walinzi hao na kuanza kuwashambulia kwa visu aina ya sime, marungu na fimbo.
Mashambulizi hayo yalisababisha walinzi Sayuni Ndika Nemes (25) na Sanula Masaga Msabila (36) kujeruhiwa. Wote ni walinzi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Turiani.
Jeshi la Polisi limewakamata Sisone Lugaso Ndabali (20), Taturo Tetetea Shangalima (28) na Likua Kaika Ndikila (21), wote wakazi wa Kijiji cha Kambala, Kata ya Mkindo, Mvomero.
Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka wafugaji kuacha kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza matumizi ya taratibu na sheria katika kudai haki.
Mwisho.
.jpg)

No comments:
Post a Comment