Wazazi watakiwa kulea ndoto za watoto wao - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 30 September 2026

Wazazi watakiwa kulea ndoto za watoto wao



Wahitimu darasa la saba mwaka 2026 katika shule ya awali na msingi ya Arusha Alliance

 


Na Mwandishi wetu, Arusha


Wazazi wametakiwa kuhakikisha wanazisimamia na kuzilea ndoto za watoto wao tangu wakiwa katika ngazi ya familia, ikiwa ni pamoja na kuwapatia malezi bora, kuwaongoza katika maadili mema na kuwahimiza kumtegemea Mungu katika maisha yao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi ya Arusha Alliance, Elimboto Mdiu, wakati akizungumza katika mahafali ya 17 ya shule hiyo yaliyofanyika jijini Arusha.

Mdiu amesema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji muhimu yatakayowawezesha kufikia ndoto zao, pamoja na kusimamia maendeleo yao ya kielimu na kitabia.

Amesema ndoto za mtoto zinapaswa kuanza kulelewa tangu akiwa katika mazingira ya familia, huku wazazi wakitakiwa kuwafundisha watoto maadili mema yatakayowasaidia kuwa raia wema katika jamii.

Mdiu pia amesisitiza umuhimu wa kuwafundisha watoto kumcha na kumtegemea Mungu, akieleza kuwa malezi ya kiroho ni sehemu muhimu katika kuwajenga watoto wenye misingi mizuri ya maisha.

Kwa upande wa shule hiyo, Mdiu amesema wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi ubunifu mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kutumia vipaji na uwezo wao katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi katika mahafali hayo, Profesa Nuhu Khatibu, Bw. Mishita Ezra, amesema jamii inapaswa kutambua kuwa kumaliza darasa la saba si mwisho wa safari ya elimu, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kielimu.

Ezra amesema wazazi wanapaswa kutambua kuwa safari ya elimu ni ndefu na hivyo wanapaswa kuendelea kuwaunga mkono watoto wao katika hatua mbalimbali za masomo yao.

Amesema wahitimu hao wanapaswa kutumia kipindi cha miezi mitatu kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani kujijenga katika maadili mema, nidhamu na tabia zinazofaa.

Ameongeza kuwa elimu inapaswa kwenda sambamba na malezi, kwani mtoto anahitaji kuwa na nidhamu na maadili mema pamoja na maarifa ya darasani ili aweze kuwa mwanajamii mwenye mchango chanya.

Jumla ya wanafunzi 114 wamehitimu darasa la saba katika Shule ya Awali na Msingi ya Arusha Alliance kwa mwaka huu.

No comments: