AOMBA MSAADA BAADA YA MIEZI MINNE BILA KULA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 15 October 2026

AOMBA MSAADA BAADA YA MIEZI MINNE BILA KULA





Na Lilian Kasenene, Morogoro


 Maipacarusha20@gmail.com


Hassan Bryton (56), mkazi wa Mkata, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, anaomba msaada wa wasamaria wema ili aweze kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi, baada ya kukaa zaidi ya miezi minne bila uwezo wa kula kutokana na uvimbe kwenye koo.


Hassan, ambaye kwa sasa anategemea dripu ili kupata maji mwilini, ameshindwa kuendelea na shughuli yake ya kuchoma na kuuza mkaa iliyokuwa ikimpatia kipato kutokana na hali yake ya kiafya. Hali hiyo imemfanya ashindwe kujigharamia matibabu anayohitaji.


Licha ya kuandikiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, bado hajafanikiwa kufika huko kutokana na ukosefu wa fedha za kugharamia safari na mahitaji mengine yanayohusiana na matibabu.


Akizungumza kwa shida kutokana na hali yake, Hassan anasema tatizo hilo limebadili maisha yake kwa kiasi kikubwa, kutoka mtu aliyekuwa akijitafutia kipato kupitia kazi yake hadi kutegemea msaada wa wengine katika kukidhi mahitaji ya msingi.


Kwa sasa anaishi na dada yake, Amina Mohammed Malenda, mjane mkazi wa Mtaa wa Mgaza, Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro, ambaye amejitwika jukumu la kumhudumia licha ya kukabiliwa na changamoto zake za maisha.


Amina anasema hali ya ndugu yake inahitaji msaada wa haraka, akieleza kuwa uwezo wake wa kifedha ni mdogo huku mahitaji ya mgonjwa yakiendelea kuongezeka siku hadi siku.


Anasema familia inakabiliwa na ugumu wa kumudu gharama za matibabu na mahitaji mengine, wakati Hassan anatakiwa kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi baada ya kupewa rufaa katika Hospitali ya Jeshi ya Mzinga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.


Katika jitihada za kupunguza makali ya changamoto hiyo, baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mgaza wamekuwa wakichangishana fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kununua dripu na kugharamia mahitaji mengine ya msingi ya mgonjwa. Hata hivyo, michango hiyo bado haitoshi kukidhi mahitaji yote yanayomkabili Hassan.


Mmoja wa mabalozi wa Mtaa wa Mgaza, Ifrahim Kaunya, maarufu kama Teacher, anafahamu hali ya familia hiyo pamoja na juhudi zinazofanywa na wananchi katika kumsaidia Hassan.


Hassan hana mke wala mtoto, hivyo dada yake ndiye anayemhudumia kwa sasa. Kutokana na hali hiyo, familia inaomba wadau mbalimbali, taasisi na wananchi wenye uwezo kujitokeza kumsaidia ili aweze kufika Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.


Kwa yeyote atakayeguswa na hali yake na kutaka kumsaidia, mchango unaweza kutumwa kupitia dada yake, Amina Mohammed Malenda, kwa namba ya Airtel 0684037960.


Msaada wowote, kulingana na uwezo wa mchangiaji, unaweza kuwa hatua muhimu katika kumwezesha Hassan kupata huduma za afya anazohitaji.


......

No comments: