Wanawake vijijini nguzo ya uchumi, watakiwa kutumia nishati safi. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 15 October 2026

Wanawake vijijini nguzo ya uchumi, watakiwa kutumia nishati safi.

 






Juslime Marco,Monduli.


maipacarusha20@gmail.com 


Mkuu wa Wilaya ya Monduli Gloriana Kimath,amesema mwanamke wa kijijini ni kiungo muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuinua pato la taifa, uzalishaji wa chakula na usalama wake, mifugo, malezi ya watoto na ujasiriamali.


Kimath ameyasema hayo Leo Octoba 15,2026  wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kushiriki maadhimisho ya siku ya mwanamke wa kijijini, maadhimisho yaliyofanyika katika Kata ya Lepurko, kijiji cha Nanja, Mkoani Arusha

Amesema Serikali inatambua nafasi ya mwanamke wa kijijini kufikia dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. “Mwanamke alikuwa hamiliki ardhi, hakuweza kuchangia mada na wanaume na hakuwa akichaguliwakuwa kiongozi, kwa zama hizi mabadiliko ni makubwa kwa kuwa wanawake wana mchango mkubwa ndani ya jamii” Amesema Kimath


Aliongeza ya kwamba, Wanawake wa kijijini zaidi ya 200 kwa siku za hivi karibuni wamekabidhiwa hati za umiliki wa ardhi katika kata ya Naalarami na Engaruka na Amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ga Monduli, kuhakikisha kata ya Lepurko pia wanawake wakabidhiwe hati hizo za umiliki wa ardhi.


Kimath amewaasa wanawake kuachana na matumizi ya nishati inayoharibu mazingira badala yake wawe vinara wa matumizi ya nishati safi kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan alivyo mstari wa mbele kupigania matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira.

Katika kuhakikisha wanawake wa kijijini wanawajibika kwa malezi ya watoto wao, Kimath amewaomba akina mama kuhakikisha hawavumilii watoto wa kiume kuacha shule mara baada ya kupelekwa jando maana limekuwa tatizo kubwa ndani ya jamii na linawaharibu watoto kabla hawajafikia ndoto zao.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ambaye ndiye mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii Wilaya ya Monduli, amesema katika kuadhimisha siku hii muhimu, mwanamke wa Kijijini anategemewa sana ndani ya Taifa katika Usalama na Uhifadhi wa chakula, Ustawi wa familia na Uhifadhi wa mazingira huku akiwasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo.


Akizungumzia Maadhimisho hayo,Mkurugenzi wa taasisi ya wanawahabari ya kusaidia jamii za Pembezoni(MAIPAC),Mussa Juma amesema katika kufikia mapinduzi ya nishati Safi na Salama wanawake ni wadau muhimu.


Juma amesema MAIPAC inakusudia kuzindua mradi wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi Kwa wanawake wa jamii za pembezoni.


"Tunaamini wanawake wakipata elimu ya nishati Safi na utunzwaji wa mazingira jamii itakuwa Salama zaidi"amesema


Juma anasema wapo Latika za mwisho za kushirikisha wadau mbalimbali ili kufanikisha Mradi huo.


Mwisho

No comments: