![]() |
| NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Magawa Madele |
![]() |
| Wanafunzi wa SUA wakimsikiliza NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Magawa Madele |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Maipacarusha20@gmail.com
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Magawa Madele, ameitaka sekta ya mifugo kuongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka asilimia sita ya sasa, akisema Tanzania ina fursa kubwa ya kiuchumi kutokana na wingi wa mifugo iliyopo nchini.
Dkt. Madele alisema hayo wakati akizungumza katika Sherehe za 43 za Utoaji wa tuzo na Zawadi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ikijiandaa na Sherehe za 48 zitazofanyika chuoni hapo Morogoro.
Alisema Tanzania ina zaidi ya ng’ombe milioni 40, zaidi ya mbuzi milioni 20 pamoja na mifugo mingine, hivyo rasilimali hiyo inapaswa kutumika kwa tija zaidi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
![]() |
Kwa mujibu wa Dkt. Madele, ongezeko la mchango wa sekta ya mifugo linahitaji kuwekeza zaidi katika kuongeza tija, ubunifu, utafiti, teknolojia na uzalishaji wa bidhaa zenye thamani katika mnyororo mzima wa mifugo.
Alisema wataalamu na wadau wa sekta hiyo wana wajibu wa kuhakikisha wingi wa mifugo uliopo nchini unageuzwa kuwa fursa ya kiuchumi kwa kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo na kuboresha uzalishaji.
Dkt. Madele, ambaye ni mhitimu wa SUA, alisema Chuo hicho kina nafasi muhimu katika kuzalisha wataalamu na tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo na kilimo kwa ujumla.
Kauli hiyo imekuja wakati SUA ikitoa tuzo 242 kwa washindi 205 katika Sherehe zake za 43 za Utoaji wa Zawadi, ikiwa ni sehemu ya kutambua ubora katika taaluma, uongozi na utafiti.
Dkt. Madele aliwataka wanafunzi waliopata tuzo kutokuchukulia mafanikio hayo kama mwisho wa safari, bali kama mwanzo wa majukumu na fursa kubwa zaidi.
![]() |
Alisema tuzo hizo ni matokeo ya bidii, nidhamu, ustahimilivu na kiu ya kutafuta maarifa, huku akiwataka washindi kukumbuka changamoto walizopitia pamoja na watu waliowaunga mkono katika safari yao ya masomo.
“Mnatambuliwa kwa mafanikio yenu. Yasherehekeeni, lakini msiyachukulie kama mwisho wa safari. Yachukulieni kama mwanzo wa majukumu makubwa zaidi na fursa kubwa zaidi,” alisema.
Alisema mafanikio ya kitaaluma hayaji kwa njia nyoofu, hivyo wanafunzi hao wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto na vikwazo vinavyoweza kujitokeza katika safari yao ya maisha.
Aidha, aliwataka kuwa wabunifu, wenye nidhamu na uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia maarifa waliyoyapata chuoni kwa manufaa ya jamii na taifa.
“Zaidi ya yote, tumieni maarifa yenu kutumikia binadamu na kujenga taifa letu,” alisema.
Dkt. Madele aliwapongeza wahadhiri, watafiti, wataalamu wa maabara na wafanyakazi wa utawala wa SUA kwa mchango wao katika kuwaandaa wanafunzi kuwa wataalamu na viongozi wa taifa.
Pia alizitambua familia za wanafunzi hao, akisema wazazi, walezi, wenza, ndugu na marafiki wamekuwa na mchango mkubwa kupitia msaada wa kifedha, kihisia na ushauri katika safari ya masomo.
Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, alisema tuzo hizo zimefanikishwa na mchango wa wafadhili 56 na zinajumuisha tuzo za kitaaluma 214, tuzo za uongozi 23 na tuzo tano za utafiti.
Alisema wanafunzi 45 miongoni mwa waliotambuliwa wamefanikiwa kupata zaidi ya tuzo moja, huku tuzo 18 zikitolewa kwa washindi zaidi ya mmoja.
Prof. Chibunda aliwapongeza washindi hao na kuwataka kuendeleza kiwango cha ubora walichokionesha ili kiwe msingi wa mafanikio yao katika maisha ya kitaaluma na kikazi.
Prof. Chibunda aliwashukuru wafadhili 56 waliofanikisha utoaji wa tuzo hizo, akisema mchango wao unasaidia kujenga utamaduni wa ubora miongoni mwa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo.
Alisema SUA inaendelea kuboresha mazingira ya kitaaluma kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo, unaolenga kuongeza ushindani wa taasisi hiyo na kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya jamii na soko la ajira..
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 3,309 wanatarajiwa kutunukiwa shahada katika programu 69.
Mbali na tuzo za kitaaluma, SUA pia imetambua watafiti watano kwa mchango wao katika utafiti na ubunifu, pamoja na viongozi bora wa wanafunzi waliochaguliwa kupitia mchakato wa kidemokrasia.
Chuo pia kimetoa Tuzo ya Jumuiya ya Wahitimu (Convocation) kwa Mwanafunzi Bora wa Shahada ya Umahiri (Masters), tuzo iliyoanzishwa mwaka 1989 na inayotolewa kwa kuzingatia vigezo vya kitaaluma, ikiwemo kuwa na GPA ya 4.0 au zaidi na kukamilisha masomo pamoja na kuwasilisha tasnifu ndani ya miaka miwili.
.......





No comments:
Post a Comment