WAZAZI WATAKIWA KUWAJENGA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI NA NIDHAMU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 8 October 2026

WAZAZI WATAKIWA KUWAJENGA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI NA NIDHAMU





mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


 Jamii imetakiwa kuwajenga watoto na vijana katika misingi ya uadilifu, nidhamu na maadili mema ili waweze kuwa raia wema na wenye mchango chanya katika maendeleo ya jamii.


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Shule ya St Mary Duluti, Br. Protas Mangu, wakati wa mahafali ya 17 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibuni.


Br. Mangu alisema kuwa wahitimu wa Kidato cha Nne bado wana nafasi kubwa ya kuwa watu waadilifu katika jamii, hivyo wanapaswa kutumia elimu waliyoipata kujenga maisha yenye mwelekeo mzuri.

Mkuu wa Shule ya St Mary Duluti, Br. Protas Mangu


Alisema kuwa pamoja na elimu, nidhamu ni msingi muhimu katika maisha ya kila siku, hivyo aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanaweka nidhamu katika kila hatua watakayopiga baada ya kumaliza shule.


Aidha, aliwataka kuwa na ujasiri wa kuishi maisha yanayozingatia maadili mema na kutokubali kushawishiwa kufanya mambo ambayo yanaweza kuharibu maisha yao ya baadaye.


Br. Mangu pia aliwataka wahitimu hao kuondokana na tamaa ya kutaka kujipatia mafanikio ya haraka, akisema kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu, bidii na kufuata njia sahihi.


Alisisitiza umuhimu wa kujiepusha na makundi mabaya ambayo yanaweza kuwapeleka katika tabia zisizofaa na kuwafanya kushindwa kutimiza ndoto zao za maisha.


Aliwataka wahitimu hao kuishi kama raia wema kwa kuheshimu sheria, watu wengine na kutumia elimu yao katika kujenga jamii yenye maendeleo.


Kwa upande wao, wahitimu hao kupitia risala yao iliyosomwa na Nathan Joseph, walisema shule hiyo imewapatia elimu ya darasani pamoja na elimu ya ujasiriamali ambayo itakuwa msaada mkubwa katika maisha yao ya baadaye.


Nathan alisema elimu ya ujasiriamali waliyoipata itawasaidia kuwa na weledi katika kujiajiri na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo kuwa na uwezo wa kujenga maisha na uchumi wao.


Aidha, aliwaomba wazazi na walezi kuendelea kuiunga mkono shule hiyo kwa kuwawezesha wanafunzi waliobaki kupata basi la shule, akisema usafiri huo utawawezesha wanafunzi kusafiri kwa uhuru na urahisi zaidi wanaposhiriki shughuli mbalimbali za kimasomo.

No comments: