Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
WAJUMBE wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Lucas Zacharia na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Hans Nkya wamempongeza mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Justin Nyari kwa kuwekeza shule ya Glisten inayotoa taaluma bora na kuchochea uchumi wa eneo hilo kupitia ajira.
Diwani wa Kata ya Endiamtu Lucas Zacharia akizungumza baada ya kutembelea Glisten Pre & Primary School kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo amesema Nyari ni mdau wa maendeleo mahiri hivyo anastahili pongezi.
"Hapa Mirerani tungekuwa na wadau 10 wa maendeleo kama Nyari tungepiga hatua kubwa mno ya maendeleo kwa namna ambavyo amekuwa akijitoa kwa jamii," amesema Zacharia.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Hans Nkya ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Kisimani ambapo shule ya Glisten ilipo amesema shule hiyo imeipatia sifa eneo hilo.
"Glisten Pre & Primary School ipo kwenye eneo letu na inatoa sifa kubwa kwetu kutokana na taaluma inayotoa kwani ufaulu wake mara nyingi ni wa kitaifa na tunapata pongezi nyingi," amesema Nkya.
Amesema yeye binafsi ana watoto watatu wanaosoma kwenye shule hiyo ya Glisten kwani inatoa elimu bora kwa wanafunzi kwenye hatua ya awali na msingi.
Mwenyekiti mstaafu wa mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Zaire amesema Nyari ni mtu mwenye kuipenda Mirerani na wachimbaji wengine wamuige kwa kuwekeza Mirerani.
"Kungekuwa na wadau 10 wa maendeleo wenye kuwekeza hapa Mirerani kama Nyari, hata haya maneno ya hali imekuwa ngumu yangepungua, kwani ajira zingekuwa za kutosha," amesema Kobelo.
Mjumbe wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Claudia Dengesi (Mama Sonjoo) amesema Nyari amekuwa akijitoa mara zote katika kusaidia jamii na shule ya Glisten imekuwa nembo nzuri ya Mirerani.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Glisten, Denis Costantin amewashukuru wajumbe hao wa maendeleo kwa kuwatembelea na kuungana nao siku hiyo ambayo imefanyika mahafali.
MWISHO

No comments:
Post a Comment