Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
KIKOSI cha Usalama Barabarani kimeagizwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria za usalama barabarani, kwamba ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na uzembe na kutokuzingatia sheria hizo zilizopo.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura alitoa ahizo hilo mkoani Morogoro, wakati wa kuaga miili ya askari watatu waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Oktoba 8 mwaka huu, katika eneo la Magole, wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
IGP Wambura aliwataja askari waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni G9771 SGT Abdallah Ramadhani (37), aliyekuwa dereva wa gari aina ya pickup lenye namba za usajili PT 5361 GMW, mali ya Jeshi la Polisi, pamoja na PC Rehoboan Marko (32) na PC Michael Lucian (23).
Aidha,aliwataka madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeraha kwa watu..
“Kama jeshi tumepata pigo kwa kuondokewa na askari wengi katika kipindi kifupi.hawa ni askari tuliokuwa bado tunawategemea,” alisema.
![]() |
Aliongeza kuwa askari wengi waliopoteza maisha ni vijana waliokuwa na mchango muhimu kwa Taifa na ambao walikuwa tegemeo kwa familia zao.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji, alisema askari wote saba waliojeruhiwa katika ajali hiyo wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, huku hali zao zikiendelea vizuri.
kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, alisema Jeshi la Polisi limepoteza askari mahiri na wenye uwezo mkubwa, akibainisha kuwa baadhi yao walikuwa wakufunzi wa mafunzo ya kijeshi.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment