UTAMBUZI WA MIILI YA AJALI YA GREEN LINE KUKAMILIKA KESHO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 10 October 2026

UTAMBUZI WA MIILI YA AJALI YA GREEN LINE KUKAMILIKA KESHO

 


 


Na Lilian Kasenene, Morogoro


Maipacarusha20@gmail.com


MKEMIA Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, amesema zoezi la upimaji wa sampuli kwa ajili ya utambuzi wa miili ya watu waliofariki dunia katika ajali ya basi la Green Line lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, linatarajiwa kukamilika kesho jioni.


Alisema wataalamu wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika ndani ya muda uliopangwa.



Dk Mafumiko alisema utambuzi wa miili hiyo unahusisha hatua mbili kuu, ambazo ni uchunguzi wa miili iliyopatikana na uthibitishaji wa uhusiano wa kifamilia kwa kulinganisha sampuli za marehemu na za ndugu zao, wakiwemo wazazi, kaka na dada, ili kubaini utambulisho wao kwa usahihi.


Alieleza kuwa zoezi hilo linafanyika kwa ushirikiano kati ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kwa lengo la kuhakikisha utambuzi wa marehemu unakamilika kwa wakati.


Ajali ya basi la Green Line pamoja na ajali nyingine iliyohusisha gari la Polisi na lori katika barabara kuu ya Morogoro–Dodoma zimesababisha vifo vya watu 32 na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.


Kutokana na hali hiyo, ndugu wa watu waliokuwa safarini ambao hawajapata taarifa kuhusu walipo wapendwa wao wanatakiwa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili kupata maelekezo kuhusu utaratibu wa kutoa sampuli za vinasaba kwa ajili ya utambuzi wa marehemu.


Mwisho.

No comments: