MAHAKAMA YA RUFANI KUSIKILIZA RUFAA YA KIHISTORIA KUHUSU UHURU WA MAHAKAMA NA MADARAKA YA RAIS - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 9 October 2026

MAHAKAMA YA RUFANI KUSIKILIZA RUFAA YA KIHISTORIA KUHUSU UHURU WA MAHAKAMA NA MADARAKA YA RAIS

 

Wakili Paul Kisabo 

Mwandishi Wetu, Dodoma 


maipacarusha20@gmail.com 


Leo Mahakama ya Rufani ya Tanzania jijini Dodoma inasikiliza rufani ya Wakili Paul Kisabo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Mhe. Jaji Levira, Mhe. Jaji Muruke na Mhe. Jaji Mlacha saa tatu kamili asubuhi. Wakili Paul Kisabo (Mrufani) anawakilishwa na Wakili Mwandamizi John Seka. 


Shauri hilo la rufaa namba 330 la mwaka 2023 linaibua mjadala mpana kuhusu uhuru wa Mahakama, mgawanyo wa madaraka na mipaka ya mamlaka ya kikatiba ya Rais katika uteuzi na uondoaji wa Jaji Mkuu madarakani.


Rufaa hiyo inatokana na shauri la kikatiba namba 09 la mwaka 2022 lililofunguliwa na Wakili Paul Kisabo katika Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Dar es Salaam. Katika shauri hilo wakili Kisabo aliiomba Mahakama Kuu kutamka kwamba Ibara ya 118(2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitoi sababu wala utaratibu wa namna ya kumuondoa Jaji Mkuu kwenye nafasi ya Jaji Mkuu kama mkuu wa mhimili wa Mahakama  badala yake inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mkuu wa Mhimili wa Serikali mamlaka ya kumuondoa Jaji Mkuu kwenye nafasi ya Jaji Mkuu bila hata kueleza sababu kinyume na kanuni ya mifumo ya udhibiti na uwiano wa madaraka (principle of checks and balances) na kanuni ya uhuru wa mahakama. Kwa mujibu wa mrufani, hali hiyo inaweza kusababisha hofu kuhusu uhuru wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.


Serikali, kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilipinga madai hayo na kueleza kuwa Katiba inapaswa kusomwa kwa ujumla wake. Hoja ya Serikali ilikuwa kwamba mamlaka ya Rais kuhusu kumuondoa Jaji Mkuu kwenye nafasi ya Jaji Mkuu hayawezi kutafsiriwa kwa kutegemea ibara moja pekee, bali kwa kuhusisha masharti mengine ya Katiba yanayolinda hadhi, usalama wa kazi na uhuru wa Majaji.  


Katika uamuzi wake wa tarehe 7 Machi 2023, Mahakama Kuu ilitupilia mbali shauri hilo la mrufani ambapo iliamua kuwa masharti husika ya Katiba yanapaswa kusomwa kwa pamoja. Mahakama ilieleza kuwa Jaji Mkuu, akiwa pia Jaji wa Mahakama ya Rufani, ananufaika na ulinzi wa kikatiba unaotolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani. 


Rufaa hiyo ina umuhimu wa kipekee kuhusu uhuru wa mhimili wa mahakama na kama ni sahihi mkuu wa mhimili wa serikali (Rais) kuwa na mamlaka ya kumuondoa mkuu wa mhimili wa mahakama (Jaji Mkuu) bila kutoa sababu yoyote, athari zake ukizingatia kwamba Rais na Jaji Mkuu ni wakuuu wa mihimili miwili tofauti ambayo inapaswa kuwa sawa kikatiba. Uamuzi wa Mahakama ya Rufani unatarajiwa kutoa mwongozo muhimu katika kulinda uhuru wa mahakama na usalama wa madaraka ya Jaji Mkuu nchini. 


Kwa msingi huo, wadau wa sheria, waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu, wasomi na umma kwa ujumla wanakaribishwa kufika Mahakama ya Rufaniy a Tanzania jijini Dodoma kufuatilia kwa karibu rufaa hiyo. 


No comments: