Na Mwandishi wetu, Rombo
maipacarusha20@gmail.com
Rombo. Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, amesema madereva wa bodaboda wilayani humo wote watapatiwa mafunzo bure katika chuo cha mafunzo na ufundi stadi(Veta) mafunzo ambayo yatasaidia kupunguza matukio ya ajali wilayani humo ambapo kila siku huripotiwa wastani wa matukio mawili ya ajali kwa siku.
Profesa Mkenda, ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema mafunzo hayo yatawajengea madereva uelewa wa sheria za barabarani na kulinda usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Akizungumza Oktoba 7, 2026, wakati akikabidhi vyeti kwa vijana 15 waliohitimu mafunzo ya udereva kupitia Veta, amesema mafunzo hayo yatatolewa bila malipo na kwa muda usiowaathiri katika shughuli zao za kujipatia kipato.
Profesa Mkenda amesema Serikali pia itashirikiana na wadau kuwapatia vijana elimu ya ujasiriamali, ikiwamo kuunda vikundi na kupata mikopo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Rombo, Mohammed Semfuko, amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na majeraha kwa madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Naye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Rombo, Temmy Masae, amesema mafunzo hayo yatawasaidia madereva kutambua sheria za barabarani na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za usafirishaji.
Amesema elimu hiyo pia itawasaidia madereva kutimiza masharti ya kupata leseni na kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, hivyo kupunguza changamoto wanazokutana nazo wanapokuwa barabarani.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment