Mwandishi wetu,Dar es Salaam
maipacarusha20@gmail.com
Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametoa miezi sita kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuandaa sera mahususi ya biashara bunifu (startups), itakayowezesha vijana kupata mitaji, masoko na fursa za uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza ajira na kukuza uchumi unaotegemea ubunifu na teknolojia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akifungua Wiki ya Biashara Bunifu (Startups Week) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Ndejembi amezitaka Taasisi za Fedha kuweka mifumo rafiki ya mitaji badala ya kutegemea mikopo pekee, huku akielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuanzisha kituo cha pamoja cha ubunifu (Innovation Centre) kitakachowaunganisha vijana na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
![]() |
Amesema Serikali itaendelea kufungua fursa za kiuchumi kupitia asilimia 30 ya manunuzi ya umma yaliyotengwa kwa makundi maalumu na fedha za uwezeshaji zinazofikia Sh bilioni 200, huku akisisitiza Chama cha Biashara Bunifu Tanzania kushirikishwa kikamilifu katika maandalizi ya Sera hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara si polisi wala mgambo wa kufunga biashara, bali jukumu lake ni kuhamasisha, kulea na kukuza biashara bunifu. Ameahidi kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi kuboresha Sera na Sheria zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia, huku TanTrade ikiendelea kutangaza bidhaa na ubunifu wa Watanzania katika masoko ya kimataifa.
![]() |
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameahidi kuendelea kuunga mkono biashara bunifu ili kupanua fursa za ajira kwa vijana, huku Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Bunifu Tanzania, Bw. Paul Makanza, akisema sekta hiyo imechangia kuzalisha takribani ajira 20,000 licha ya changamoto za mitaji na masoko.
Awali, Makamu wa Rais alitembelea maonesho ya wabunifu na wawekezaji, ikiwemo Benki ya NMB, mdhamini mkuu wa tukio hilo, ambayo imefanikiwa kufadhili biashara bunifu sita, huku nyingine tano zikiwa katika hatua za mwisho za uwezeshaji.




No comments:
Post a Comment