BAKWATA WAHAMASISHA MSINGI IMARA WA MAENDELEO MKOANI SINGIDA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 19 October 2026

BAKWATA WAHAMASISHA MSINGI IMARA WA MAENDELEO MKOANI SINGIDA

 

SHEKH WA WILAYA YA IRAMBA SHEIKH ATHUMANI HUSSEIN MGOMBAIKA AKIZUNGUMZA  VIONGOZI  WA KATA NA MISIKITI KATIKA KIKAO MAALUM CHA BAKWATA KILICOFANYIKA MASJID TAQWA MISIGIRI IRAMBA

 

NA SEIF TAKAZA IRAMBA SINGIDA

Jumatatu OKTOBA  19 ,2026

 

BARAZA  Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida limeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha utendaji, uwajibikaji na maendeleo ya taasisi hiyo kupitia ziara maalumu ya kimkakati iliyofanyika katika Msikiti wa Taqwa Misigiri jana   Wilayani   Iramba,  Mkoa wa Singida  ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa ziara zinazolenga kuhamasisha utekelezaji wa maelekezo ya kiutendaji, kuimarisha usimamizi wa fedha na kuweka misingi imara ya maendeleo endelevu ya BAKWATA.

 

Ziara hiyo inaakisi dhamira ya uongozi wa BAKWATA chini ya Mheshimiwa Mufti wa Tanzania,  Sheikh  Abubakar Zuberi bin Ally kwa kushirikiana na Baraza la Ulamaa Taifa, na

 

Halmashauri  kuu ya Bakwata   Taifa,  yenye lengo   la  kusimamia rasilimali zake, kuimarisha mapato na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.

 

Aidha  BAKWATA Mkoa wa Singida imeamua kuyapa uzito mkubwa maelekezo ya uongozi wa kitaifa kwa kuyafikisha katika ngazi za wilaya na kufuatilia utekelezaji wake kwa vitendo.

 

Ziara ya Iramba imeongozwa na Mwenyekiti wa BAKWATA Mkoa wa Singida,   Sheikh Omar Mughenyi akishirikiana na Katibu wa Mkoa,Sheikh Abdallah Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, makamu Katibu pamoja na wajumbe wa kamati hiyo.

 

Ujumbe wa mkoa umekutana na viongozi wa BAKWATA Wilaya ya Iramba, akiwemo Sheikh wa Wilaya, Katibu wa Wilaya na wajumbe wengine walioshiriki kikao hicho kwa lengo la kujadili

 

hatua zilizofikiwa, changamoto zilizopo na mikakati ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

 

Tofauti na ziara za kawaida za kiitifaki, ziara hizi zimejikita katika ufuatiliaji, tathmini, ushauri wa kiutendaji na kuchochea hatua za maendeleo zinazopimika. Lengo si kusikiliza taarifa pekee, bali kuhakikisha kuwa maelekezo yanageuka kuwa vitendo na vitendo vinazaa matokeo.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa BAKWATA Mkoa Sheikh  Abdallah Masudi  amehimiza viongozi wa wilaya na ngazi nyingine za kiutendaji kuzingatia maelekezo ya taasisi, kutekeleza majukumu kwa wakati na kuhakikisha kuwa kila jukumu linalopangiwa utekelezaji linafuatiliwa kwa karibu.

 

Amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, usimamizi madhubuti wa mapato na matumizi, utoaji wa

 

taarifa sahihi za kifedha na kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato yanayostahili kuingia katika taasisi.

 

Ujumbe mkuu ni kwamba maendeleo ya BAKWATA hayawezi kutegemea matarajio pekee. Yanahitaji viongozi wenye dhamira, nidhamu, uadilifu na utayari wa kusimamia maamuzi yaliyokubaliwa.

 

Viongozi wanapaswa kuelewa kuwa fedha za taasisi ni nyenzo ya kutekeleza wajibu wake wa kidini, kijamii na kiuchumi. Kwa hiyo, ukusanyaji wa mapato, matumizi yenye tija na uwazi katika usimamizi wa fedha lazima viende sambamba.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango ya BAKWATA Mkoa wa Singida  Omari Kundya amesisitiza umuhimu wa kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele, uwezo wa kifedha na

 

malengo yaliyowekwa na taasisi.

 

Kamati imeendelea kuhamasisha viongozi wa wilaya kuhakikisha kuwa mipango ya fedha haibaki kwenye maandishi, bali inakuwa mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

 

Aidha, msisitizo umewekwa katika kutambua vyanzo vya mapato vilivyopo, kubuni vyanzo vipya, kufuatilia makusanyo, kudhibiti matumizi yasiyo na tija na kuhakikisha kuwa kila ngazi inakuwa na utaratibu unaoeleweka wa kusimamia rasilimali zake.

 

Utekelezaji wa mipango unahitaji ushirikiano kati ya viongozi, watendaji na wajumbe wa kamati husika. Kila mmoja anapaswa kutambua wajibu wake katika kuhakikisha kuwa BAKWATA inakuwa taasisi yenye uwezo wa kifedha na inayotekeleza miradi yake kwa ufanisi.

 

 

Katika mjadala wa kikao hicho, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango Omar Kundya

 amesisitiza umuhimu wa viongozi wa wilaya na maeneo yao kuweka juhudi katika kutafuta na kupata ardhi kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya BAKWATA.

 

Ameeleza kuwa upatikanaji wa ardhi ni hatua muhimu katika kujenga msingi wa miradi ya muda mrefu, kuimarisha umiliki wa rasilimali za taasisi na kuweka mazingira mazuri ya kuanzisha miradi ya kiuchumi na kijamii.

BAKWATA inayotaka kuwa imara kesho lazima ianze kujenga rasilimali zake leo. Ardhi, majengo, miradi ya uzalishaji na vyanzo endelevu vya mapato ni sehemu ya msingi wa kujenga taasisi inayoweza kujitegemea na kutekeleza majukumu yake bila kutegemea michango ya dharura pekee.

 

Katika kikao hicho, Sheikh wa Wilaya ya Iramba Sheikh Athumani Husein Mgombaika amesisitiza umuhimu wa viongozi kuendelea kushirikiana katika kusimamia majukumu ya BAKWATA, kuimarisha uwajibikaji na kuweka mbele maslahi ya  Bakwata .

 

Ziara ya Iramba ni sehemu ya mkakati mpana wa BAKWATA Mkoa wa Singida wa kuzunguka wilaya zote saba za mkoa huo ili kutathmini utekelezaji wa mipango, kuhamasisha nidhamu ya fedha na kuimarisha usimamizi wa rasilimali.

 

Mfululizo huu wa ziara unaonesha kuwa Singida imeamua kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha utendaji wa BAKWATA. Ni mwanzo wa msukumo unaolenga kuifanya taasisi hiyo  kuwa yenye mipango madhubuti inayotarajiwa  kuendelea katika Wilaya ya Ikungi, ikiwa sehemu  ya  kuhakikisha  Bakwata inapata Maendeleo endelevu.

 

 

 

Ziara hizi zinatoa nafasi ya kusikiliza changamoto zinazowakabili viongozi wa maeneo mbalimbali, kubadilishana uzoefu, kutoa maelekezo na kuweka msukumo wa pamoja katika kutekeleza maamuzi yatokananayo vikao vinavyotoa maamuzi kwa mujibu wa katiba ya Bakwata.

 

Ziara ya Iramba ni ushahidi wa dhamira ya BAKWATA Mkoa wa Singida ya kuimarisha utendaji na kuendeleza safari ya kujenga taasisi yenye uwezo wa kifedha na rasilimali za kudumu.

Mwisho

 

 

 

No comments: