DCEA NA WADAU WAFANYA KONGAMANO LA KUWASAIDIA WARAIBU WANAOKINZANA NA SHERIA JIJINI ARUSHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 7 November 2026

DCEA NA WADAU WAFANYA KONGAMANO LA KUWASAIDIA WARAIBU WANAOKINZANA NA SHERIA JIJINI ARUSHA

 



Na Prisca Libaga Arusha


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi, wataalamu wa afya na mashirika ya kijamii wameungana kuimarisha mfumo wa Deflection, unaolenga kuwaelekeza watu wenye uraibu wa dawa za kulevya wanaokinzana na sheria kwenye huduma za matibabu na msaada wa kisaikolojia badala ya kutegemea adhabu pekee.


Akizungumza jijini Arusha, Kamishna wa DCEA Hussein Mbaga, aliyemwakilisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema uraibu wa dawa za kulevya ni changamoto ya kiafya inayohitaji matibabu na ushirikiano wa wadau ili kuwasaidia waathirika kurejea katika maisha ya kawaida.


Amesema mfumo huo utasaidia kupunguza uhalifu mdogo unaohusiana na dawa za kulevya, kupunguza msongamano katika mahakama na magereza pamoja na kuokoa maisha.


Kiongozi wa PTACC Afrika, Dkt. Yvonne Olando, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya polisi, wataalamu wa afya na jamii, huku akitaka kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wenye uraibu na kuufanya mfumo huo utambulike na kutekelezwa kwa viwango vinavyofanana barani Afrika.


Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Henry Mwaibambe amesema Jeshi la Polisi linaona umuhimu wa kuwabaini mapema watu wenye changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwaelekeza kwenye huduma stahiki, akibainisha kuwa kupitia mfumo wa Polisi Kata unaofikia kata 3,956 Tanzania Bara na shehia 358 Zanzibar, kuna fursa ya kuimarisha ushirikiano na jamii.


Amesisitiza pia umuhimu wa familia kutoa taarifa mapema ili watu wenye changamoto hizo wapate msaada kabla hali haijawa mbaya.


Kongamano hilo la "PTACC Africa Deflection Summit" la siku mbili, Novemba 5-6, 2026, katika Ukumbi wa Corridor Spring Hotel, limewakutanisha washiriki zaidi ya 100 wakiwemo wawakilishi wa vyombo vya sheria, taasisi za afya na mashirika ya kiraia, kujadili njia za kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, kukabiliana na overdose na kuimarisha mifumo ya kuwaunganisha waathirika na huduma za matibabu.


Ujumbe mkuu: Wenye uraibu wanahitaji msaada, matibabu na ushirikiano wa jamii ili kurejea katika maisha ya kawaida badala ya kuwafunga pekee.


#kataa_dawazakulevya_timiza_malengo_yako

No comments: