NDEGE WAHARIBIFU NA NZIGE WATISHIA UZALISHAJI WA CHAKULA AFRIKA MASHARIKI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 16 November 2026

NDEGE WAHARIBIFU NA NZIGE WATISHIA UZALISHAJI WA CHAKULA AFRIKA MASHARIKI

 

Meneja wa Usimamizi wa Visumbufu vya Mlipuko wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Godfrey Kirimbo,

Mkurugenzi wa DLCO Moses Mwesigwa

Meneja wa DLCO upande wa Tanzania , Didas Moshi

Na Lilian Kasenene, Morogoro


Maipacarusha20@gmail.com 


Uwezo wa ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea na wadudu wanaohama, wakiwemo nzige wa jangwani na viwavi jeshi, kushambulia mazao kwa makundi makubwa umeendelea kuwa tishio kwa uzalishaji wa chakula katika nchi za Afrika Mashariki.


Hali hiyo imeongeza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utambuzi wa mapema wa maeneo yaliyo katika hatari ya kushambuliwa, ili kuwezesha hatua za udhibiti kuchukuliwa kabla visumbufu hivyo havijasababisha hasara kubwa kwa wakulima.


Wataalamu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia wamekutana mjini Morogoro katika mafunzo ya kikanda yanayolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia ya anga katika kufanya uchunguzi, kufuatilia na kudhibiti ndege na wadudu hao waharibifu.


Mafunzo hayo ya siku nne yameandaliwa na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani katika Afrika Mashariki (Desert Locust Control Organization for Eastern Africa – DLCO-EA), kwa ushirikiano na Benki ya Waarabu kwa Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (Arab Bank for Economic Development in Africa – BADEA).


Akizungumzia mikakati ya kukabiliana na visumbufu hivyo, Mkurugenzi wa DLCO-EA, Moses Mwesigwa, alisema shirika hilo linaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za ufuatiliaji na udhibiti.


Alieleza kuwa matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) ni miongoni mwa teknolojia zinazoweza kusaidia katika shughuli za udhibiti, ikiwemo kupulizia viuatilifu katika maeneo yaliyoathirika.


Kwa upande wake, Meneja wa DLCO-EA nchini Tanzania, Didas Moshi, alieleza changamoto zinazokabili juhudi za kudhibiti visumbufu hivyo pamoja na hatua zinazochukuliwa kukabiliana nazo.


Naye Meneja wa Usimamizi wa Visumbufu vya Mlipuko wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Godfrey Kirimbo, ameeleza maeneo yanayokabiliwa na changamoto kubwa zaidi na mikakati ya Serikali katika kukabiliana na mashambulizi ya ndege na wadudu hao.


Aidha, mafunzo hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama kupitia kubadilishana taarifa, utaalamu na teknolojia, kwa kuzingatia ukweli kwamba ndege na wadudu wanaohama hawazuiliwi na mipaka ya nchi.


Ushirikiano huo unatajwa kuwa muhimu katika kuwezesha hatua za pamoja za kudhibiti mashambulizi, kulinda mazao, kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Mwisho.

No comments: