Rais Samia: Mageuzi nishati safi yaboreshe maisha ya wananchi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 12 November 2026

Rais Samia: Mageuzi nishati safi yaboreshe maisha ya wananchi

 




Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendeleza mageuzi ya nishati safi kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira katika sekta za usafirishaji, kilimo na viwanda, hatua inayolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kuongeza ufanisi wa nishati na kufungua fursa za uwekezaji na ajira.


Akizungumza katika tukio la ngazi ya juu kuhusu kuendeleza mageuzi ya sekta ya nishati Tanzania na matumizi ya nishati safi ya kupikia katika shule na taasisi za afya, lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) jijini Antalya, Uturuki, Rais Samia amesema juhudi hizo zinajumuisha kuimarisha matumizi ya magari yanayotumia umeme na gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) katika sekta ya usafirishaji, sambamba na kuongeza uzalishaji wa umeme ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya nchi.


Amesema Tanzania inatambua kuwa mageuzi jumuishi ya nishati hayaishii katika kuongeza uzalishaji wa umeme pekee, bali yanapaswa pia kubadili namna wananchi wanavyoishi na kufanya shughuli zao za kila siku, kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia safi na endelevu.


Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema nishati safi ya kupikia ni miongoni mwa ajenda muhimu alizochagua kuzisimamia kwa lengo la kuboresha maisha ya wanawake na watoto, si nchini Tanzania pekee bali pia katika bara la Afrika, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanajikwamua na athari zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi. #TanzaniaCOP31

No comments: