WAENDESHA BODABODA NA WAJASIRIAMALI WANUFAIKA NA MIKOPO KITETO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 27 November 2026

WAENDESHA BODABODA NA WAJASIRIAMALI WANUFAIKA NA MIKOPO KITETO

 


Na Mwandishi wetu, Kiteto 


MBUNGE wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau ameongoza shughuli ya kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na kugawa pikipiki kwa vikundi vya waendesha bodaboda (maofisa usafirishaji)


Ole Lekaita akizungumza kwenye ugawanyaji huo uliofanyika chini ya mti mjini Kibaya, amesema zaidi ya vijana wa bodaboda 80 wamenufaika kwa kupatiwa mikopo ya pikipiki, vikundi vya wanawake, wafugaji wamenufaika na mradi wa ufugaji wa ng'ombe wa maziwa.


Amesema mafundi wa magari wamepatiwa zabuni ya kutengeneza magari ya Serikali baada ya kupata mkopo wa asilimia 10 wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto.


Amesema kupitia mikopo hiyo vijana watakuwa wanajishughulisha ili kupata kipato na kuondokana na matukio ya uhalifu na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.


"Nimefurahishwa na juhudi za makundi haya na utaratibu mzuri na namna mikopo hii ilivyotolewa na kila kata itaguswa, hongereni sana," amesema Ole Lekaita.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Athumani Msimbazi amesema kupitia mikopo hiyo jamii itanufaika kwani Kiteto ya sasa ni ya maendeleo siyo ile ya zamani ya migogoro.


Afisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Irene Mosha amewaasa wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia vyema ili wapate faida na kurejesha mikopo.


Wanufaika wa mikopo hiyo waliokabidhiwa pikipiki, hundi na vifaa vingine, vikundi vya waendesha bodaboda, mafundi magari, vijana, wanawake wajasiriamali na watu wenye ulemavu wamemshukuru Mbunge wao kwa kupata mikopo hiyo.


Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo Awadh Haji amemshukuru Ole Lekaita kwa kuwakabidhi mikopo hiyo ambayo ataitumia ipasavyo ili apate faida na kisha kuirejesha mkopo.


Mwanamke mjasiriamali Rehema Mwamidi amesema mikopo hiyo itawanufaisha wanawake na kuwaongezea kipato tofauti na awali.


MWISHO

No comments: