|
Baadhi ya waandishi wa Habari wakiwa katika picha ya pamoja na Tume ya Haki za Binadamu nchini mara baada ya kusikiliza hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu
|
|
Mussa Juma Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi Mkoani Arusha akieleza hali ya ukiukwaji wa haki za Binadamu Kwa waandishi wa habari Ngorongoro
|
|
Mkurugenzi wa Pingos Forum Edward Porokwa akieleza ukiukwaji wa haki za binadamu kwa tume ya haki za binadamu nchini ilipokutana na kundimla waandishi wa Habari Mkoani Arusha
|
|
Profit Mmanga mwandishi wa Habari wa Wasafi Media Mkoani Arusha akieleza tume ya haki za Binadamu nchini namna alivyokamatwa mara baada ya kuandika habari za wananchi wa Ngorongoro na kuhakiwa na Runinga yake ya Mtandaoni
|
NA: Andrea Ngobole, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Katika utekelezaji wa kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania leo Tume ya haki za
binaadamu na Utawala bora nchini (THBUB), imekutana na waandishi wa
habari mkoani Arusha, waliowahi kuathirika baada ya kuandika habari za mgogoro wa ardhi wa
Loliondo na Ngorongoro.
Tume hiyo iliyopo katika ziara ya kutembelea wilaya ya Ngorongoro kufahamu uwekaji wa mipaka Loliondo na kuhamishwa kwa wakazi wa Ngorongoro kwenda Msomera kama kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, imeamua kukutana
na wanahabari waliowahi kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za
binaadamu, baada ya kupokea wito kutoka wa asasi za kutetea haki za
binaadamu mkoani Arusha.
|
Jaji
mstaafu Mathew Mwaimu (upande wa kushoto) ambaye ni mwenyekiti wa Tume
ya Haki za Binadamu nchini akisikilza maelezo ya baadhi ya waandishi
waliokumbwa na madhila ya ukiukwaji wa haki za Binaadamu baada ya
kuandika habari za Ngorongoro na Loliondo
|
Mwenyekiti
wa tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu, alisema walikuwa
Loliondo na Ngorongoro kuwasikiliza wananchi na wakapata maombi kuja
kuwasikiliza na wanahabari ambao kwa namna moja ama nyingine wameathirika
na matukio ya Loliondo na Ngorongoro.
|
Lilian Oddo akiielezea Tume ya Haki za Binadamu alivyokamatwa na Polisi baada ya kuandika habari zinazohusu masuala ya Loliondo |
|
Wakizungumza
na tume hiyo, wanahabari Julius Msagati(star Tv), Lilian Oddo( Leo Tv)
na Profit Mmanga( Wasafi TV) walieleza tume hiyo waliwahi kukamatwa na kuwekwa
rumande kutokana na kuandika habari za Ngorongoro.
Msagati
alisema mnamo mwezi june mwaka jana, akiwa na waandishi wengine,
walialikwa na wananchi katika kijiji cha Nainokanoka ndani ya eneo la
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na baada ya mkutano na wananchi
walikamatwa na askari wa mamlaka hiyo.
"Tulikamatwa
tukapekuliwa kwa zaidi ya masaa matano bila kuelezwa makosa yetu na
baada ya mlalamiko kufika ngazi mbali mbali tuliachiwa saa nne usiku
kutoka Ngorongoro"alisema
Mwanahabari Oddo na Mmanga walieleza kukaa rumande kituo kikuu cha polisi Arusha,
kitengo cha Utalii kwa siku mbili baada ya kukamatwa kutokana na
kuandika habari za wananchi kuhusiana na zoezi la kuhamishwa wananchi wa
tarafa ya Ngorongoro kwenda Msomera.
"tulikamatwa
maeneo tofauti kama wahalifu na kupelekwa polisi na tuliandika maelezo,
lakini baada ya siku mbili tulitolewa na Waziri wa mambo ya ndani,
Hamad Masauni ambaye alikuwa kwenye ziara Arusha hasa baada ya
malalamiko ya wanahabari"alisema
Alisema licha ya kuachiwa Runinga yake ya mtandao aliyokuwa anaisimamia ya Leo Tv iliondolewa mtandaoni.
|
Mwandishi
wa habari mwandamizi wa Star TV mkoani Arusha, Angelo Mwolekwa akieleza
hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika kukuasanya taarifa za
wakazi wa Ngorongoro na Loliondo
|
Mwandishi
mwandamizi wa star tv, Angelo Mwoleka alisema wakati wa zoezi la
kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro na kumegwa eneo la loliondo
kuanzishwa pori la akiba Pololeti kumekuwepo na ukiukwaji wa haki za
binaadamu.
Mwoleka
alisema wanahabari walikuwa wakipokea simu ya vitisho kutoandika habari
za wananchi na badala yake waandishi maalum walipewa jukumu la kuandika
habari za upande mmoja tu na hivyo kuwanyima haki watanzania wengi
kujua ukweli.
Mkurugenzi
wa shirika la Uraia na msaada wa kisheria(CILAO) Odero Charles aliomba
tume hiyo, kutenda haki katika sakala hilo kwani kuna matukio mengi ya
ukikwaji haki za binaadamu ikiwepo wananchi kuporwa ardhi na mmoja
kupotea.
"Tunaimani
kubwa na tume hii kutoa taarifa ya haki ambayo itakwenda kuondoa tatizo
la migogoro ya ardhi hasa pale ambapo serikali inakiuka sheria na
kuchukuwa ardhi ya wananchi bila maridhiano kwa madai ya kufanya
uhifadhi ama kuwapa wawekezaji"alisema.
Tume
ya Haki za binaadamu na Utawala bora imefika Arusha na kutembelea
Loliondo na Ngorongoro, ikiwa ni takriban miezi mitatu tangu tume ya
afrika ya haki za binaadamu nayo kutembelea maeneo hayo kuzungumza na
wananchi kuhusiana na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binaadamu.
No comments:
Post a Comment