Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Wakati Serikali ikiwa imeingiza shehena ya Sukari, kwa nia ya kuondoa uhaba wa sukari uliopo nchini, kiwanda cha Sukari cha Mkulazi Kilichopo Wilayani Kilosa kimeanza rasmi zoezi la kusambaza bidhaa hiyo mitaani ili kupunguza makali ya bei yanayowakabili wananchi maeneo mbalimbali.
Usambazaji huo wa sheheza ya sukari kwa matumizi ya majumbani kwa mara ya kwanza tumeanza na kiwanda cha Mkulazi tangu kuanza uzalishaji wake.
Afisa mwandamizi wa masoko na mauzo kutoka Kampuni hodhi ya Mkulazi Milkasia Joseph, amebainisha hayo wakati wa zoezi la upakiaji wa Sukari ya ujazo wa kilogram 25 ambayo imeanza kuingizwa rasmi sokoni kwa mkoa wa Morogoro.
Milkasia amesema Sukari hiyo imekidhi viwango vya ubora wa hali juu baada ya bidhaa hiyo kupitishwa katika vipimo vyote kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo imelengwa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kiungo katika aina mbalimbali za mapishi yanayotajwa Kwenda kuwafurahisha watumiaji wa sukari hiyo sokoni.
“Zoezi la kuuza Sukari tumeanza, na kuanza kupakia kwenye magari ya wateja ambayo yamefika kiwandani kwetu, Kwa sasa tayari tumesha ainisha wateja wetu,Watanzania wote ambao ni wafanyabiashara tunawakaribisha kufanyakazi na sisi, Kuingiza Sukari yenye ubora wa hali ya juu wa hali ya juu sokoni, kwaajili ya kuisadia nchi yetu na kupunguza nakisi ya Sukari,” amesema Milkasia.
Afisa uhusiano wa Kampuni hodhi ya Mkulazi Clementina Patrick amesema wamejipanga vyema kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia Watanzania wote kwa bei elekezi za Serikali ili kuwapunguzia watumiaji wa bidhaa hiyo machungu kutokana na mfumuko wa bei uliosababishwa na uhaba wa sukari mtaani.
“Kama mnavyoona leo ndio siku ya Kwanza tunaingiza bidhaa yetu ya sukari sokoni, kwa sasa tumeanza na sukari ya majumbani (Brown Sugar) na tunatarajia hapo baadae kuzalisha pia na sukari za viwandani, Sukari yetu tunaiuza kwa bei elekezi kwa Wafanyabiashara,"amesema.
Pia amesema wanatarajia kuwafikia Watanzania kwa bei elekezi ya Serikali ili kuwapunguzia Wananchi makali,”amesema Clementina Patrick.
Naye Meneja wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi Mhandisi Aaron Mwaigaga amesema kiwanda hicho kinaendelea na zoezi la uchakataji wa sukari ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo mtaani unaosababishwa na mvua zinazondelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.
Mhandisi Mwigaga amesema Mkulazi imejidhatiti kuendelea kupeleka sukari sokoni licha ya changamoto za mvua zinazoendelea lakini pale hali ya hewa inapotulia watajitahidi kuendelea na zoezi la uchakataji wa Sukari ili kupunguza nakisi ya sukari kwa wananchi kama ambavyo malengo ya Serikali yalivyo katika kupunguza makali ya bei kwa jamii.
Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ni Kiwanda Kipya kinachomilikiwa kwa ubia wa hisa asilimia 96 kutoka kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na hisa asilimia 4 zinazomilikiwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza (SHIMA) ambapo kilianza Uzalishaji wa majaribi ya sukari yake mwezi Disemba 2023.
No comments:
Post a Comment