ROYAL TOUR YAINUFAISHA HIFADHI YA TAIFA MIKUMI KUPATA WATALII WENGI KUTOKA ZANZIBAR WANAOTUMIA NDEGE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 9 February 2024

ROYAL TOUR YAINUFAISHA HIFADHI YA TAIFA MIKUMI KUPATA WATALII WENGI KUTOKA ZANZIBAR WANAOTUMIA NDEGE

 





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Uanzishwaji wa filamu ya Royal Tour uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kutangaza utalii wa ndani pamoja na kufunguka kwa fursa zaidi za utalii visiwani Zanzibar kumewezesha watalii wengi zaidi kutembelea hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa siku kwa kutumia ndege kwenda na kurudi.


Aidha wastani wa ndege zinazobeba abiria kati ya watano hadi hamsini zimekuwa zikitua uwanja wa ndege wa Kikoboga uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kila siku, na wakati mwingine ndege hizo kuacha kundi moja la watalii na kufuata kundi jingine na baadaye kwa awamu kuwarudisha watalii hao Zanzibar kuendelea na utalii mwingine ikiwemo wa fukwe.


Wadu wa utalii ambao wamekuwa wakifanya Kampeni ya Twenzetu Mbugani, inayolenga kuhamasisha watanzania kutembelea hifadhi za Taifa zilizopo, wametembelea uwanja huo wa ndege, ambao uko kwenye mipango zaidi ya kuboreshwa na kupanuliwa zaidi, na kukuta watalii 226 walioshuka kwa ndege kwenye uwanja huo.


Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa kitengo cha Utalii katika hifadhi ya taifa ya Mikumi, Afisa mwandamizi mkuu Herman Mtei amekiri wimbi hilo kubwa la utalii kusababishwa na kampeni ya Rais ya Royal Tour na kufunguka kwa fursa za utalii Zanzibar, na kwamba wengi wa watalii wamekuwa wakija hifadhini hapo kufanya utalii na baadaye kurudi visiwani.


Akifafanua maboresho ya uwanja wa ndege wa Kikoboga, Mhifadhi Mtei Amesema awali uwanja huo wa ndege ulikuwa na uwezo wa kupokea ndege zenye kubeba Kati ya watu watano(5) hadi kumi na tatu(13), tofauti na sasa.


Akabainisha sio wageni kutoka nje pekee walioongezeka kutembelea hifadhi ya Mikumi, bali pia watanzania wamehamasika na kuongezeka maradufu zaidi, na sasa idadi yao inawapita au kushabihiana na ya wageni kutoka nje ya nchi.


Kwa mujibu wa Mtei, hifadhi hiyo katika kipindi cha Julai 23 mwaka jana hadi Januari 30 mwaka huu, watalii walioingia hifadhini hapo walikuwa 76,620 na kati yake 38,586 ni watanzania na 38,034 wakiwa wageni kutoka nje ya nchi.


Aidha mwaka 2022/2023, waliingia wageni 109,112 wakiwemo 59,979 watanzania huku mwaka huu wa fedha hadi kumalizika mwishoni mwa Juni, hifadhi hiyo inakusudia kuvunja rekodi kwa kuingiza watalii 123,000.


"Uongozi wa hifadhi ya Mikumi umekuwa ukiongeza mikakati mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya barabara na uwanja wa ndege ili kuwafanya watalii kutembelea hifadhi hiyo bila vikwazo vya kufika kwa njia ya anga, Reli na  barabara,"amesema Mtei.


Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Augustino Masesa amesema amewaomba watanzania kutembelea hifadhi hiyo kufanya utalii wa ndani kutokana na kufika kwa urahisi kwa njia ya barabara na anga.


Masesa amesema Tanzania kutumia fursa zilizopo kuendelea kutembelea hifadhi hiyo aliyodaikika kirahisi kwa ndege, Barabara ya lami, Reli ya TAZARA na ikiwa mbioni kufikika kwa treni ya mwendo kasi SGR pindi ikianza kazi.


Akawahimiza kutumia sikukuu mbalimbali ikiwemo Sikukuu ya wapendanao (Valentine Day) inayofanyika Februari 14  kufika Mikumi kufurahia maisha ambapo mtalii wa kitanzania anaweza kupanda basi na kupokelewa lango kuu na kujionea mandhari ya hifadhi hiyo ambapo Kati ya saa moja hadi masaa mawili watakuwa wameona wanyama wengi, karibu wote ikiwemo Simba, Twiga, tembo, Kiboko, nyati na wengine.


Balozi wa mazingira nchini, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele, aliyekutwa hifadhini hapo, amesema hakuna gharana kubwa kwa mtanzania kutembelea hifadhi ya Mikumi, kula au kulala hivyo watanzania wasifikiri kufanya utalii ni kwaajili ya wageni kutoka nje Peke yao.



No comments: