SIMANJIRO YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 39 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 10 February 2024

SIMANJIRO YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 39

 



Na: Mwandishi wetu, Simanjiro


maipacarusha20@gmail.com


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamepitisha kiasi cha shilingi bilioni 39 kwa ajili ya mapendekezo ya mpango wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025.


Ofisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Happynes Masatu akisoma bajeti hiyo amesema itakidhi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo na mifugo.


Masatu amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia muongozo wa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2023/2024 na ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2020/2025.


Amesema pia imelenga mpango wa maendeleo wa Taifa kwa miaka mitano, malengo ya maendeleo endelevu 2030 na dira ya Taifa kwa mwaka 2025.


Amesema katika sekta ya afya bajeti hiyo itahakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji dawa na vifaa tiba.


"Katika sekta ya elimu tutahakikisha tunaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye shule zote za msingi na sekondari kwa kujenga, kukarabati na kumalizia madarasa, mabwani, nyumba za walimu na vyoo," amesema Masatu.


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amewasihi madiwani hao kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa watumishi wa halmashauri katika utekelezaji wa bajeti hiyo.


"Twendeni tukatekeleze bajeti hii kwa manufaa ya wananchi wetu kwani lengo ni kuhakikisha wanafanikiwa kupitia miradi itakayoanzishwa katika maeneo yao," amesema Kanunga.


Mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka, amesema bajeti hiyo itawanufaisha wananchi wa eneo hilo kwani kata nyingi zimeguswa katika sekta tofauti.


"Kupitishwa kwa bajeti ni hatua moja na kutekelezwa kwa bajeti ni hatua nyingine hivyo madiwani na watumishi wapeane ushirikiano katika kufanikisha," amesema Ole Sendeka.


Diwani wa Kata ya Ruvu Remit, Yohana Maitei (Kadogoo) amesema bajeti hii imekuwa na matumaini kwa upande wa sekta ya afya, elimu, kilimo na mifugo.


Diwani wa kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer amesema anatarajia bajeti hii itaboresha zaidi miundombinu ya elimu kwani iliyopita ilifanikisha ujenzi wa madarasa mapya ya shule ya sekondari Simanjiro.


Diwani wa kata ya Loiborsoit, Siria Baraka Kiduya amesema bajeti ya mwaka huu imeinufaisha kata yake kwani itapata madarasa mawili shule shikizi ya Songoyo na darasa moja shule ya msingi Losokonoi.


Diwani wa Kata ya Terrat, Jackson Ole Materi amesema wananchi wa eneo hilo wameshapiga kura kwa Rais Samia Suluhu Hassan wanasubiria kudumbukiza kwenye boksi kwani wamepata kituo cha afya na zahanati kila kijiji.



No comments: