SERIKALI YATOA BIL4.6 KUPELEKA UMEME MAENEO YA MIGODENI RUVUMA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 22 August 2024

SERIKALI YATOA BIL4.6 KUPELEKA UMEME MAENEO YA MIGODENI RUVUMA

 

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha mauzo ya madini ya makaa ya mawe kutoka katika Kijiji cha Paradiso Halmashauri ya Mbinga.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa kituo cha mauzo ya madini ya makaa ya mawe kutoka katika Kijiji cha Paradiso Halmashauri ya Mbinga Mussa Haji akisoma taarifa ya mgodi mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Nishati Judith Kapinga.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji Cha Paradiso waliofika kwenye uzinduzi wa kituo cha mauzo Cha madini ya makaa ya mawe.


Na Mwandishi wetu,Mbinga


maipacarusha20@gmail.com 


SERIKALI imetoa kiasi cha sh bilioni 4.6 kwaajiri ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi mkoani Ruvuma ambapo kiasi cha sh milioni 280 zimepelekwa katika mgodi wa Market Insight Limited (MILCOAL) uliopo Kijiji cha Paradiso Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani humo.


Akizungumza kwenye uzinduzi wa kituo cha mauzo cha makaa ya mawe ya Kampuni ya Market Insight Limited Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga alisema  tayari wameanza kupeleka nguzo na kuvuta waya ambapo ndani ya mwezi mmoja umeme utakuwa umefika katika eneo la mgodi.


Aliupongeza Uongozi wa Market Insight Limited kwa jitihada  za kuendelea kuimarisha utulivu ndani ya mgodi kiuchumi na uwezeshwaji wa kiuchumi kupitia fursa zinazopatikana ikiwemo fursa za ajira kwani uwekezaji huo unaendelea kuchochea uchumi wa Taifa.


"Nawapongeza sana MILCOAL kwa kuendelea kuwekeza na kuweza kutoa fursa mbalimbali kwa ajiri ya kuendeleza uwekezaji mgodi kwani wao ni mfano mzuri  wa Makampuni yanayofanya vizuri kwenye kuendeleza fursa za uwekezaji nafahamu vituo vya usambazaji wa madini ya makaa ya mawe  vipo mbali na migodi pamoja na sababu zingine moja wapo ni changamoto ya barabara natambua kuwa kama uwekezaji wa mwanzoni mliweka mazingira mazuri ikiwemo kufungua barabara kutoka sehemu ya kijiji cha Mtunduwalo hadi Luwimbi kwa gharama ya sh. Milioni 800" alisema Naibu Waziri wa Nishati Kapinga.


Alisema japo barabara inayokwenda kwenye migodi ya makaa ya mawe bado inachangamoto lakini wanatambua jitihada za mwanzoni ambazo zimewanufaisha watu wengi ikiwemo wawekezaji wengine wa migodi na kwamba serikali inaendelea kukwamua ujenzi wa barabara hiyo lakini pia barabara zote zinazoingia katika maeneo ya migodi ambapo Waziri wa Ujenzi alishafika katika eneo hilo na amewahakikishia swala la barabara hiyo linaendelea kufanyiwa kazi na wakati wowote kuanzia sasa shughuli za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha rami utaanza.


Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga alisema kuwa sekta ndogo hiyo ya makaa ya mawe ina mchango mkubwa sana katika usalama wa Nishati katika uwekezaji wa viwanda vya ndani na nje ya Nchi ambapo amesema kuwa halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni mojawapo ya maeneo muhimu sana yanayochangia katika uwekezaji kupitia madini hayo kwa kiasi kikubwa tunafurahi kuwa chanzo cha nishati thabiti na ya kutegemewa katika maeneo ya uwekezaji mkubwa hususani viwandani .


"Serikali ya awamu ya sita inathamini uwekezaji kupitia wizara ya nishati inayo miradi inayotekelezwa ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya makubwa ya uwekezaji ikiwemo migodini ambapo wiki iliyopita Naibu Waziri mkuu na Waziri wa nishati Dkt. Doto Biteko alifungua kituo cha kupoza umeme katika mgodi mkubwa wa GGM pamoja na mgodi huu tunayo miradi mingi ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya uwekezaji ikiwemo migodi. " alisema Naibu Waziri Kapinga.


Awali akisoma taarifa ya mradi huo mwakalishi wa Kampuni ya Market Insighht Limited Mussa Hadji alisema kuwa Kampuni yao ilianza rasmi shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe 2017katika Wilaya ya Mbinga  mkoani Ruvuma kwa lengo la kuchangia kikamilifu katika sekta ya madini nchini kupitia uchimbaji na uuzaji wa makaa ya mawe ambapo tangu kuanzishwa Kwake kampuni hiyo imejipambanua kwa kuzalisha na kusambaza makaa ya mawe yenye ubora wa hali ya juu kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.


Kwa upande wake kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Peles Magiri alisema kupitia usimamizi thabiti wa serikali miundo mbinu muhimu kama ya barabara na usambazaji wa umeme katika maeneo ya migodi vimeendelea kuboreshwa hali ambayo itarahisisha uendeshaji wa shughuli za kibiashara na kuboresha upatikanaji wa Nishati kwa huraisi .


Naye Diwani wa Kata ya Rwanda Dougras Mwingira alisema  kampuni hiyo ya MILCOAL imeshatoa ajira kwa wakazi wa kata ya Rwanda jambo ambalo limeongeza kwa kiasi kikubwa uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambayo imekuwa ikikusanya mapato kupitia kwenye migodi ya makaa ya mawe iliyopo wilayani humo.


Naye Stephan Komba mkazi wa Kijiji cha Paradiso aliiomba serikali kupitia Wizara ya Madini kuyashinikiza makampuni yanayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe kuhakikisha kuwa kwenye barabara zinazotoka kwenye migodi hadi kwenye maeneo ya makazi ya watu zinamwagiwa maji mara kwa mara kwa lengo la kupunguza vumbi inayosababishwa na magari yanayosafirisha makaa ya mawe kutoka migodini hadi kwenye kituo cha mauzo ya makaa ya mawe.


Mwisho.

No comments: