DC KAGANDA AAGIZA HATI YA MWEKEZAJI BABATI VIJIJINI ICHUNGUZWE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 24 April 2025

DC KAGANDA AAGIZA HATI YA MWEKEZAJI BABATI VIJIJINI ICHUNGUZWE

 





Na Epifania Magingo,Manyara 


maipacarusha20@gmail.com 


Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda àmetoa agizo kwa ofisi ya Mkurugenzi Babati Vijijini pamoja na idara inayoshughulikia masuala ya ardhi kufuatilia na kuifuta hati ya mwekezaji ambaye anamiliki ardhi yenye  hekta 24 kinyume na Sheria badala ya kumiliki ekari 24 halali ambazo amekodishiwa na wanakijiji wa olasit kata ya Nkaiti Kwa lengo la kufanya Uwekezaji.


Inaelezwa kuwa wanakijiji hawanufaiki na chochote Kutokana na mwekezaji huyo kwenda kinyume na sheria ya umiliki wa ardhi huku ikidaiwa kuwa ameshindwa kutimiza matakwa ya Kijiji na kusudi la kupewa ardhi hiyo ikiwa pamoja na kuweka kempu ambazo ingekua ni kichocheo kwa wageni kuja na kupata mapato ya Kijiji na Serikali.


Kaganda ametoa agizo hilo alipokuwa Kijijini hapo  wakati akizungumza na wazee wa eneo hilo pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazokabili kijiji Cha Olasit ikiwemo kero  ya utolewaji wa huduma ya afya kusua sua katika Kituo Cha Afya Cha Nkait huku akiigaiza TAKUKURU kwenda kuchunguza utendaji kazi wa Kituo hicho pamoja na kuagiza kwa kuletwa kwa dawa muhimu.


" Suala la  dawa tusifanye mchezo,yale majengo yanakua hayana maana kama hakuna huduma muhimu kwa hiyo DMO panga utaratibu mzauri, wazee si mmemsikia DMO eeh natoa siku mbili tu dawa zipatikane na wazee mfuatilie mtanipa taarifa kama huduma hiyo mnaipata". amesema Kaganda 


"Izo hekta amekata na hati, hiyo hati amepata wapi!!!sasa hili lisichukue muda mrefu, ndani ya wiki Moja Mkurugenzi na jopo lako la ardhi mje hapa mfuatilie, na hiyo hati ifutwe na apewe alichopewa na Kijiji tu,na nataka nijue ni nani amempa hiyo hati". amesema Kaganda 


Kaimu Mkurugenzi Babati Vijijini Godfrey Jafar Balaza amekiri kuifahamu changamoto ya mwekezaji huyo kwa kumiliki eneo hilo kinyume na Sheria na kuahidi kwamba  Ofisi ya Mkurugenzi Italishughulikia suala hilo kwa haraka kama ilivyoagizwa.


"Mtendaji alishaniletea nyaraka, na inaonekana huyu mwekezaji alipewa ekari 24 tu na Kijiji, lakini yeye kwenye hati yake inaonesha ni hekta 24 maana yake hapo sasa ni mara mbili ya ekari zaidi ya 50, kwa hiyo tutalifanyia kazi".amesema Godfrey 


Aidha, Kaganda pia, ametoa rai kwa wananchi wanaoishi maeneo karibu na Hifadhi ya Wanyama Pori kutafuta fursa zilizopo katika Uwekezaji pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji walioko maeneo hayo ili kukuza Uchumi katika ngazi ya Jamii na Taifa kwa ujumla.

 

"Sasa badala ya kuona uhifadhi ni adui, Uwekezaji ni adui, tutafute fursa tuangalie jinsi ambavyo sisi tunaweza kutumia yale mahoteli na wageni wanaokuja kujitengenezea kipato cha mmoja mmoja, mimi nimekuja na moja tu ilo la kuku, sasa mnaweza mkafuga woote hapa mliopo na msitosheleze soko, amesema Kaganda 


Amesema Uhifadhi na Utalii umesaidia kuongeza pato la Taifa kwa kiasi kikubwa na kwamba wanakijiji wanapaswa kuchangamkia fursa ya kuwasomesha Vijana wao katika vijiji hivyo ili waweze kunufaika na Utalii na Uwekezaji ambao unafanyika ndani ya Taifa.


Katika kusikiliza kero hizo kwenye kijiji Cha Olasit Mkuu wa Wilaya Kaganda, amesema wapo baadhi ya watu wanafanya upotoshaji kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo litarudisha maendeleo nyuma.


"Nimeona kuna upotoshaji mwingi sana unaendelea, nimesikia kuna mambo huku mengi ya uwongo yameelezwa, mmeambiwa Serikali imekataza wakina mama kukata minyaa katika misitu, jambo ambalo sio kweli".amesema Kaganda 


" Vijiji hivi kukiwa na utulivu WMA inaweza kutengeneza fedha nyingi sana ambazo mtafanyia maendeleo, itategemea tu mmechagua viongozi ambao sio wabinasfi, sasa mwenyekiti kwenye suala GMP ni mpango bora wa ardhi, kwa hiyo mkiwa na eneo lazima muweke mpangilio mzuri wa ardhi na kinachofanyika saivi ni kupanga mpango bora wa matumizi katika eneo lote ambalo linalozunguka vijiji hivyo kumi". 


Pia, Kaganda akatoa ufafanuzi kuhusu kero ya Wanyama Pori tembo na fisi kuvamia makazi ya watu na kuharibu mazao ni kwamba mwarobaini wake tayari umeshapatikana kwakua wanasubiri Wizara iweze kutoa kibali Cha kujenga uzio wa kuzuia Wanyama kuvamia mazao.


Ukumbukwe kuwa hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Babati Kaganda aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa chama kwenda  katika Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara, kwa lengo la kujifunza kuhusu utekelezaji wa uzio wa umeme unaozunguka maeneo ya hifadhi na vijiji jirani hii ilitokana  kufuatia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Babati kuhusu tembo na wanyama wengine wakali wanaoharibu mazao, kuleta hofu, na kuathiri shughuli za kiuchumi.

No comments: