Na Queen Lema Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka taasisi zote zinazojihusisha na ununuzi wa umma kuhakikisha zinakuza ununuzi endelevu unaochochea usawa wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi na uendelevu wa kimazingira nchini.
Dkt. Gwajima ametoa wito huo leo Juni 14, 2025, jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la 9 la Ununuzi wa Umma, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Ununuzi wa Umma wa Kidigitali kwa Maendeleo Endelevu, Ukuzaji wa Kampuni za Wazawa na Makundi Maalum kwa Ukuaji wa Uchumi Jumuishi.”
Katika hotuba yake, Dkt. Gwajima amesema taasisi za umma zina wajibu mkubwa kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya muda mrefu ya wananchi kwa kuzingatia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.
Amesisitiza kuwa taasisi za ununuzi lazima zitenge asilimia 30 ya zabuni zao za mwaka kwa kampuni za wazawa na makundi maalum kama wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wazee ili kuchochea ushiriki wao katika maendeleo ya kiuchumi.
“Taasisi hizo zikitoa zabuni kwa wazawa zikiwemo kampuni za wanawake, vijana na walemavu, zitawezesha sekta ya ununuzi kukua zaidi,” alisema Dkt. Gwajima na kusisitiza kuwa taasisi hizo zisimamie utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Aidha, halmashauri zote nchini zimeagizwa kuunda vikundi maalum vya vijana, walemavu, wanawake na wazee katika maeneo yao ili viweze kushiriki kwenye mchakato wa maombi ya zabuni kupitia mfumo wa kidigitali wa NeST.
Akizungumzia umuhimu wa matumizi ya TEHAMA katika sekta ya ununuzi wa umma, Dkt. Gwajima alisema:
“Tanzania kama ambavyo nchi nyingi duniani imetambua umuhimu wa matumizi ya TEHAMA katika ununuzi wa umma ambapo mifumo hii kwa kiasi kikubwa inaondoa changamoto ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwenye sekta mbalimbali.”
Alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki kama NeST yameleta mapinduzi makubwa katika sekta ya ununuzi kwa kupunguza gharama, makosa, athari kwa mazingira na kuongeza kasi ya ununuzi na uwazi katika mchakato wa zabuni.
“NeST imeongeza uwazi na uwajibikaji, imechangia kuleta thamani halisi ya fedha inayotumika katika ununuzi lakini pia mfumo huu unaleta faida nyingi na kuimarisha utawala bora pamoja na kuongeza wigo wa ushindani. Na zaidi imesaidia mapambano dhidi ya rushwa, uzembe, udanganyifu na madhaifu katika ununuzi wa umma,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Denis Simba alisema mfumo wa NeST ulianza kutumika rasmi Julai 1, 2023 na hadi sasa una moduli sita muhimu ikiwemo e-registration, e-tendernet, na e-contract ambayo inatarajiwa kuanza kutumika rasmi Julai 2025.
“Hapa tunazungumzia ujenzi wa shule darasa moja, ujenzi wa madundu ya vyoo, ununuzi wa bandari, ununuzi unaofanyika kwa wenzetu wa reli, ununuzi wa meli na ununuzi ambao unagusa maeneo mbalimbali,” alisema.
Amebainisha kuwa hadi kufikia Juni 11, 2025, jumla ya wazabuni 38,163 wameidhinishwa na kusajiliwa katika mfumo huo ambapo 36,377 ni wazabuni wa ndani na 1,786 ni kutoka nje ya nchi.
“Pia taasisi za ununuzi 61,415 zikiwemo taasisi kuu na za ngazi ya chini za serikali za mitaa zimesajiliwa katika mfumo wa NeST, zikiwa na jumla ya watumiaji 131,202 waliothibitishwa,” aliongeza Simba.
Kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,500 kutoka sekta mbalimbali, likiwa ni jukwaa muhimu la kujadili maboresho ya mifumo ya ununuzi wa umma nchini kwa kuzingatia maendeleo ya kidigitali na ushirikishwaji wa makundi maalum katika ukuaji wa uchumi jumuishi.

No comments:
Post a Comment