![]() |
| NAIBU katibu Mkuu Wizara ya Fedha Jenifa Christian Omolo |
![]() |
| Kamishna idara ya sera za manunuzi Wizara ya Fedha Dk Frederick Mwakibinga |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
NAIBU katibu Mkuu Wizara ya Fedha Jenifa Christian Omolo amewataka maafisa masuhuli wa taasisi za umma na Halmashauri zote nchini kusoma na kuielewa vyema sheria ya manunuzi sura namba 410 ili kuhakikisha mnyororo wa ugavi unasimamiwa kikamilifu kwa maslahi ya umma.
Omolo ameagiza hayo mkoani Morogoro alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya mnyororo wa ugavi kwa wahariri wa vyombo vya habari yaliyolenga kuwajengea uelewa wahariri hao.
Omolo alisema Sheria hiyo imefanyiwa marekebisho hivi karibuni na iwapo maafisa masuhuli watasimamia kikamilifu wataweza kununua vitu kwa kufuata sheria na kuzingatia thamani ya fedha pamoja na kutoa huduma kwa wananchi.
"Tumerekebisha hii sheria na tumezijengea uwezo kila halmashauri, ununuzi ni jambo dogo katika kipengere cha mnyororo wa ugavi,unaponunua lazima uwe na mpango wa kuhakikisha kuwa mali unayonunua mwananchi anaona faida yake,"alisema.
Alitolea mfano kuwa ukinunua dawa unahakikisha zile dawa zinahifadhiwa, kutunzwa, kusambazwa na kuhakikisha zinafika kwenye zahanati husika kwamba huo ndio mfano wa mnyororo wa ugavi.
Aliongeza “lakini hata ukinunua magari hakikisha magari hayo yanatumika vizuri,lakini kwanza tunayahifadhi, kuyasajili,unayatunza ndo yatumike kwa ajili ya kuleta faida, na yakichoka lazima uwe na mpango wa kuyaondosha,”.
Naibu katibu mkuu huyo alisema maafisa masuhuli wasipofuata sheria ya ugavi mali za serikali zinaweza zikatelekezwa, zikaharibika, zikapotea ama zisitumike na kuwafikia wananchi kama ilivyokusudiwa na kwamba kila kinachonunuliwa kwa fedha ya serikali lazima kiwanufaishe wananchi.
Pia alieleza kuwa seriakli imekuwa ikipata hasara kutokana na kutofuatwa kwa misingi na sheria ya manunuzi,madhara mengine mfano wananchi kutofikishiwa dawa.
Kamishna idara ya sera za manunuzi Wizara ya Fedha Dk Frederick Mwakibinga alisema kununua ni sehemu ndogo ya mwanzo ya mnyororo wa ugavi na kwamba vitu vinaponunuliwa wapo walengwa ambao wamelengwa kupata vitu hivyo au huduma hiyo, hivyo baada ya kuimarisha ununuzi wa umma inabidi kuimarishwa kwa huduma nyingine zilizomo kwenye mnyororo wa ugavi.
“Mmesikia kupitia kazi zenu ni namna gani ununuzi wa umma unaweza kusaidia kuokoa fedha za serikali kwa kununua na kutumia njia sahihi zilizowekwa kununua kwa uangalifu,na umakini, lakini baada ya hapo na ununuzi je?mna nafasi ya kuhoji kinachoendelea kwenye mali hizo,"alisema.
"Maana yake ni kwamba zile shughuli zinazoambatana na mnyororo wa ugavi kuanzia zinaponunuliwa mpaka zinapofika kwa mlaji wa mwisho ambaye mtanzania,”alisema.
Aidha Dk Mwakibinga alisema lengo kubwa la mnyororo wa ugavi ni kwamba unaponunu vifaa vya umma kiwango,idadi na ubora uwe uleule na usiobadilika mpaka kwa mtumiaji wa mwisho na kuwa jambo hilo limekuwa na changamoto kubwa kwenye suala zima la manunuzi.
Alisema, hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wa kina na uwezo mahususi wa kufikisha taarifa sahihi na kwa wakati kwa wananchi ili kuweza kuwapa uelewa mpana umma wa Tanzania kuhusu mnyororo wa ugavi.
Aidha alisema fedha zinazotumika kwenye shughuli za manunuzi ya umma kwa maana ya ununuzi wa vitu na hduma ni fedha za watanzania na kodi na wakati mwingine fedha hizo zinapatikana kwa njia ya mikopo na vyanzo vingine ambavyo serikali inagharamia, sasa ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri na zinakwenda kumfikia aliyelegwa ni vyema shughuli za mnyororo zikaimarishwa.
Akizungumza kwa niaba ya wahariri, mwenyekiti wa mafunzo hayo Ben Mwang’onda alipongeza wizara ya fedha kwa kuandaa mafunzo hayo na uwepo wake utaleta tija na kwamba kwa kuwa wizara hizo ndio injini ya uchumi wa nchi kwa kuwa ndio inapanga mikakati ya maendeleo.
Mwisho.




No comments:
Post a Comment