Na mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), imewataka Watanzania kuendelea kushikamana na misingi ya Taifa, hususan katika kipindi hiki ambacho nchi inatafakari matukio ya vurugu za Oktoba 29, 2025 kupitia Tume iliyoundwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Alhamisi Januari 22, 2026 na Mwenyekiti wa MNF, Joseph Butiku, wakati wa kikao chake na wazee, kilichojadili masuala mbalimbali ikiwemo vurugu za Oktoba 29, mabadiliko ya Katiba, uzalendo, haki, amani na uwajibikaji.
Amesisitiza umuhimu wa kutafakari yaliyotokea kwa utulivu, busara na kwa kuzingatia misingi iliyoijenga Tanzania.
Butiku amesema matukio ya Oktoba 29 ni msiba ulioligusa Taifa zima na kwamba katika nyakati kama hizo, ni muhimu jamii kuendelea kuzungumza kwa hekima.
Amefananishia hali hiyo na msiba ambao wakati mwingine maziko yanachelewa, lakini katika kusubiri, mazungumzo yanapaswa kuendelea kwa utulivu.
Amesema wakati Taifa linajiuliza nini kilitokea Oktoba 29, kwa nini kilitokea na nani aliyesababisha, ni muhimu Watanzania wasipoteze mwelekeo wala kujikuta wakitawaliwa na lugha za matusi na jazba, hususan katika mitandao ya kijamii.

No comments:
Post a Comment