Na mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwake, Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, ataongoza upandaji wa miti utakaofanyika Januari 27, 2026 maeneo ya Bungi Kilimo Kizimkazi, Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Januari 22,2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bakari Machumu shughuli hiyo imepewa kauli mbiu ya ‘uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti’.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, zoezi hilo maalumu la upandaji miti linaakisi dhamira ya Rais Dkt Samia katika kuendeleza ajenda ya Taifa ya uhifadhi na utunzajï wa mazingira,ikiwemo upandaji miti na ulinzi wa vyanzo vya maji.
Pia, zoezi hilo linaakisi kuimarisha uoto wa asili, na kuchangia kwa vitendo juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Zoezi hili ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja na linatoa fursa kwa kila mmoja, kwa nafasi yake na mahali alipo, kushiriki katika kulinda na kuenzi mazingira kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha Rais Dkt Samia anatoa wito kwa Watanzania kuendelea kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa hiari, wakitambua kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi wa uhai, maendeleo, na usalama wa Taifa.
“Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inawahimiza wananchi, taasisi na wadau wa mazingira kuunga mkono dhamira ya Dkt Samia kwa kuendeleza ajenda ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda angalau mti mmoja nyumbani,
shuleni, kazini, au kwenye maeneo ya jami,” imeeleza taarifa.


No comments:
Post a Comment