CHUSA MINING LTD YAJENGA WODI YA MAMA NA MTOTO MIRERANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 1 February 2026

CHUSA MINING LTD YAJENGA WODI YA MAMA NA MTOTO MIRERANI

 







Na Mwandishi wetu, Mirerani 


maipacarusha20@gmail.com


KAMPUNI ya Chusa Mining LTD kupitia Mkurugenzi wake Joseph Mwakipesile, imefanikisha miradi mbalimbali ya kuwajibika kwa jamii (CSR) mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ikiwemo ujenzi wa wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya Mirerani.


Fundi msimamizi wa ujenzi wa wodi ya wanawake, watoto na ofisi katika kituo cha afya Mirerani, Abdalah Said anaeleza kuwa hatua iliyopo hivi sasa ni jengo hilo limefikia hatua ya lenta.


"Mbao za kupanua zipo tayari kwa hiyo baada ya siku tatu upauzi utaanza kwani tunamalizia kufunga baraza kwa kumimina," amesema Abdallah.


Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani Rachel Njau ametoa wito kwa wamiliki wa migodi na wachimbaji wa madini ya Tanzanite, kuipenda Mirerani na kuwezesha miradi ya CSR ili kurudisha kwa jamii pindi wanapozaliwa madini.


Ameishukuru kampuni ya Chusa Mining LTD, kwa ujenzi wa wodi ya wanawake na watoto ambayo ipo kwenye hatua ya lenta kisha kupauliwa, kuweka bati na kukamilisha .


Ameeleza kwamba mwaka jana 2025 kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mke wa mkurugenzi huyo Sporah Mwakipesile alitoa ahadi ya kununua viti mwendo 10 vya watoto wenye uhitaji maalum katika shule ya msingi Tanzanite iliyopo kata ya Mirerani.


"Viti mwendo 10 vimeshaletwa na vipo Mirerani na  magodoro 20 ya watoto wenye mahitaji maalum nayo yamenunuliwa na vitanda 60 vya watoto hao vipo tayari kwa fundi zinamalizwa,


Diwani wa kata ya Mirerani Salome Nelson Mnyawi amemshukuru Sporah Mwakipesile kwa kuwasaidia watoto hao wenye mahitaji maalum.


"Tunamshukuru sana Chusa na mke wake kwa kufanikisha hayo kwani nimeshapata taarifa kuwa viti mwendo, magorofa na vitanda vipo tayari kwa ajili ya makabidhiano kwa watoto wetu wenye mahitaji maalumu,," amesema 


Amesema wadau wengine wa maendeleo waige mfano wa Chusa Mining LTD katika kusaidia jamii inayowazunguka kupitia CSR.


MWISHO

No comments: