ZARA TOURS YANG’ARA TENA SERENGETI AWARDS KWA TUZO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 6 February 2026

ZARA TOURS YANG’ARA TENA SERENGETI AWARDS KWA TUZO

 




Na Queen Lema,Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Kampuni ya utalii ya Zara Tours yenye makao yake makuu mjini Moshi bado imeendelea kuwa Bora katika sekta ya utalii mara baada ya kuondoka na tuzo kwenye usiku Wa tuzo za Serengeti awards,


Aisha ushindi huo ni muendelezo wa mfululizo wa tuzo ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizipata karibu kila mwaka,kutokana na kufanya kazi kwa kiwango cha kimataifa zaidi.


Tuzo hiyo ilikuwa miongoni mwa tuzo 51 zilizotolewa katika hafla kubwa iliyofanyika wiki iliopita katika Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha.


Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye aliipongeza sekta ya utalii kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira, pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa kama kivutio bora cha utalii.


Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wadau binafsi umeendelea kuleta matokeo chanya, hasa katika kuboresha miundombinu na huduma zinazowawezesha watalii kupata uzoefu bora wanapotembelea vivutio vya nchi.


Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Zara Tours, Bi. Zainabu Ansell, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa ya timu, mshikamano wa ndani ya kampuni na ushirikiano mzuri kati ya serikali na wadau wa sekta ya utalii.


Alieleza kuwa maboresho yanayoonekana katika Mlima Kilimanjaro ni ushahidi wa wazi wa jitihada za pamoja za kulinda na kuendeleza rasilimali za taifa.


“Mazingira ya mlima yameimarika, huduma zimeboreshwa na hali ya usalama imeongezeka kwa kiwango kikubwa, jambo linalowapa watalii uzoefu wa kipekee,” alisema Bi. Zainabu.


Kwa mujibu wa Bi. Zainabu, Mlima Kilimanjaro umeendelea kuwa alama muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa, na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa vinara wa utalii wa mlima barani Afrika na duniani kwa ujumla.


Alibainisha kuwa ongezeko la watalii wanaopanda mlima huo limechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii na kuongeza mapato ya taifa. Kampuni kama Zara Tours zimekuwa na jukumu muhimu katika kuhakikisha wageni wanapata huduma salama, zenye ubora wa hali ya juu na zinazokidhi viwango vya kimataifa.


“Ninajivunia sana mafanikio haya. Leo ni siku ya kusherehekea hatua tulizofikia. Mimi pamoja na timu yangu tumejipanga kikamilifu kuendelea kuboresha viwango vya kitaaluma, kuongeza ubunifu na kuhakikisha wageni wengi zaidi wanavutiwa kuja kuupanda Mlima Kilimanjaro,” alisisitiza.


Bi. Zainabu aliahidi kuwa Zara Tours itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kukuza utalii endelevu, kulinda mazingira na kulitangaza taifa la Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Hafla ya Serengeti Awards imelenga kutambua na kuthamini mchango wa taasisi, makampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini  na ushindi wa Zara Tours ni kielelezo cha ubora unaoendelea kuijenga taswira ya Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.


Mwisho

No comments: