![]() |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Wanawake wametakiwa kutumia kikamilifu fursa za masomo na mafunzo zinazotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kujijengea uwezo na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya jamii.
Wito huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, wakati wa hafla ya kuwapongeza wanawake wa chuo hicho katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Prof.Muhairwa amesema chuo hicho kina mfumo thabiti wa kulinda wanawake na wasichana pamoja na kutekeleza mpango mkakati wa kulinda haki za kijinsia, hatua ambayo imechangia kuwepo kwa mazingira ya utulivu chuoni hapo.
Mwenyekiti wa Chama Cha wafanyakazi wa taasisi ya Elimu ya juu, sayansi, teknolojia, Ufundi stadi,habari na utafiti(RAAWU)tawi la SUA, Faraja Kamendu, na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu(THTU)tawi la SUA, Nickson Mkilamwene, walisema kuwapa wanawake nafasi katika kazi kunasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji katika taasisi mbalimbali.
![]() |
Viongozi hao pia waliwahamasisha wanawake kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya chuo hicho na kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kulinda maslahi yao.
Akisoma hotuba kwa niaba ya wanawake wa chuo hicho, Farida Mkongwe aliishukuru menejimenti ya chuo kwa kutoa fursa za mafunzo kwa wanawake, akisema hatua hiyo imechangia kuongeza ujuzi, uwezo na weledi wa wanawake katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Aliongeza kuwa utoaji wa mafunzo kwa watumishi unazingatia mipango na bajeti ya chuo, huku akiiomba menejimenti kuendelea kuongeza fursa hizo ili kuwajengea wanawake uwezo zaidi katika nyanja mbalimbali za kitaaluma na kiutendaji.
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Fulwe, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alisema mkoa huo umeendelea kuwa kinara katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kama sehemu ya kutambua mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Aidha, Malima alikemea tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali kuvumilia vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake, hususan wanapopoteza wenza wao, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua kali ili kulinda haki za wanawake.
Mwisho.




No comments:
Post a Comment