Shule ya msingi Bright, Moshi yajenga Maktaba ya kisasa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 27 April 2026

Shule ya msingi Bright, Moshi yajenga Maktaba ya kisasa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi

 

Ofisa Elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi, Gaudence Assey akiwa pamoja na uongozi wa shule hiyo wakikata utepe katika jengo la maktaba hiyo ya kisasa iliyopo shuleni hapo.

Wanafunzi wa shule ya msingi Bright, iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Moshi wakiwa maktaba wakijisomea.


Na Mwandishi Wetu, Moshi


maipacarusha20@gmail.com 


Moshi. Wakati Serikali ikiendelea kuboresha mitaala mbalimbali ya elimu nchini, Shule ya Msingi Bright iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, imechukua hatua ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kujenga maktaba ya kisasa.


Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Mdhibiti ubora wa elimu wa halmashauri hiyo, Neema Silayo, wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo, amesema kuwa maktaba hiyo itakuwa nyenzo muhimu katika kukuza taaluma ya wanafunzi wa shule hiyo.


“Maktaba hii itakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hivyo kuongeza ufaulu na maendeleo ya wanafunzi wetu kitaaluma,  tunategemea ufaulu wa shule ya Bright utaongezeka na ufanisi katika elimu utaimarika,” amesema 


Aidha, aliwataka wanafunzi kuitumia fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii na nidhamu pamoja na kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.


"Ni rai yangu kwa wanafunzi kutumia maktaba hii ya kisasa kwa nidhamu na kuhakikisha wanaitunza ipasavyo,” amesema


Aidha, aliwataka wazazi na jamii kuendelea kushirikiana na shule katika kuboresha mazingira ya elimu, ikiwemo miundombinu, ili watoto waweze kupata elimu bora.


Naye Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Gaudence Assey amesema uwepo wa maktaba hiyo ni fursa kwa wanafunzi kujiongezea maarifa nje ya masomo ya darasani.


“Tumeagiza kila shule iwe na sehemu ya wanafunzi kujiongezea maarifa. Watu hupenda sehemu yenye huduma bora, na zipo shule zinazodorora kutokana na kukosa huduma hizo,” alisema.


Assey aliwataka walimu kuendelea kuhakikisha usalama wa wanafunzi hasa katika kipindi hiki chenye changamoto mbalimbali za kijamii.


“Ni muhimu kulinda watoto wetu wakati wote, ikiwemo wanapokuwa safarini, kwa kuhakikisha wanakuwa chini ya uangalizi mzuri,” alisisitiza.


Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Fidel amesema shule ina wanafunzi 615 kuanzia darasa la awali hadi la saba, huku akieleza dhamira yao ni kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na kufaulu kwa viwango vya juu.


Amesema katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, shule hiyo ilishika nafasi ya tano kiwilaya kwa kupata ufaulu wa daraja A.


Pamoja na mambo mengin, Mwalimu Mkuu huyo, amesema changamoto zinazokabili shule hiyo kuwa ni baadhi ya wazazi kuchelewesha ulipaji wa ada, hali inayosababisha ugumu katika uendeshaji wa shule hasa kutokana na kupanda kwa gharama za maisha ikiwemo bei ya mafuta na bidhaa muhimu.


Mwisho.

No comments: