WADAU WAASWA KUENEZA ELIMU YA MAADILI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 30 June 2026

WADAU WAASWA KUENEZA ELIMU YA MAADILI

 



Na Lilian Lucas, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


WADAU wa utoaji elimu kwa umma wamehimizwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kuelimisha wananchi kuhusu maadili ili kudhibiti vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa misingi ya uongozi bora.


Wito huo umetolewa na Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Omar Juma, wakati wa kikao cha wadau wa utoaji elimu kwa umma kilichofanyika mkoani Morogoro.


Kamishna Mwangesi alisema mafanikio ya kuimarisha maadili hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa wadau mbalimbali wanaohusika na utoaji wa elimu kwa umma.


"Kidole kimoja hakivunji chawa. Tunahitaji kubadilishana mawazo na wataalamu wa utoaji elimu kwa umma ili kupata mbinu bora zitakazowezesha elimu ya maadili kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi," alisema.


Alibainisha kuwa changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele katika utoaji wa elimu ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka kwa maslahi binafsi, mgongano wa maslahi, rushwa, upendeleo, ukosefu wa uwazi na uwajibikaji katika maamuzi, kutotoa taarifa sahihi kwa umma pamoja na ukiukwaji wa maadili ya kazi na misingi ya uongozi bora.


Kwa upande wake, Omar Juma alisema wadau wa utoaji elimu kwa umma wana nafasi muhimu ya kuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi katika kujenga uelewa na kuimarisha utamaduni wa kuzingatia maadili.


Alisema Sekretarieti inaendelea kutumia njia mbalimbali kufikisha elimu kwa umma, zikiwemo mikutano, maonesho, machapisho, vyombo vya habari, semina na makongamano, ili kuhakikisha ujumbe wa maadili unawafikia wananchi wengi zaidi.

 





...

No comments: