![]() |
| Bicon zilizopo shambani kwa akili kuwekewa katika mashamba hayo |
Mwandishi wetu.Arusha.
maipacarusha20@gmail.com
Wamiliki wa Ardhi na Makazi eneo la Kitongoji cha Relini na Mariton, kijiji cha Malula Kata ya Malula Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, wameomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati kuzuia Uvamizi wa ardhi yao zaidi ya hekali 3000 unaofanywa na Halmashauri ya Meru.
Wananchi hao, wamesema baadhi yao licha ya kushinda kesi mahakama ya rufaa na wengine kesi zikiwa bado zipo mahakamani, wameshangazwa na uamuzi wa halmashauri kuvamia eneo hilo kuanza kupima na kuweka bicon wakitumia polisi kuimarisha ulinzi katika ardhi yao.
Halmashauri Yakiri kuvamia ardhi na licha uwepo wa kesi.
Hata hivyo, Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Jonathan Kiama akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru, kuhusiana na mgogoro huo, licha ya kukiri uwepo wa kesi Mahakama na kesi nyingine kumalizika katika mahakama ya rufaa kwa familia ya Okash kukabidhiwa ardhi, alisema ardhi hiyo ni mali ya halmashauri na sio ya wananchi.
"Sisi tunapima na kuweka alama eneo la halmashauri kwani hakuna zuio lolote la mahakama tusifanye hivi, ni kweli kulikuwa na kesi mahakama kuu kati ya familia ya Ahmed Okash na wananchi 83, mahakama kuu iliwapa ushindi familia ya Okash lakini halmashauri tumepeleka maombi namba 157/02/2022 mahakama ya rufaa kuomba marejeo ya kesi kwani walioshitakiwa kuvamia ardhi na kushindwa hawakuwa wamiliki"alisema
Hata hivyo, hoja hiyo imepingwa na wakili wa wananchi hao, Wakili Fridolin Gwemelo ambaye alitaka halmashauri kuheshimu mahakama na kauli za mara kwa mara za Rais Samia Suluhu na Jaji Mkuu, George Masaju kuheshimu uhuru wa mahakama na kuacha vitendo ambavyo vinagombanisha serikali na wananchi.
"Kesi tayari ilikwisha Halmashauri imeomba mapitio ya kesi mahakama ya rufaa na kuongezewa muda wa kuwasilisha maombi ya kujumuishwa katika kesi hiyo, sasa wamekwenda kuvamia ardhi ambayo kisheria sio mali yao huku ni kudharau mahakama "alisema
Wananchi ambao ardhi yao imevamiwa wamlilia Rais Samia.
![]() |
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wamiliki wa ardhi hiyo, watoto wa marehemu Ahmed Okash, wakiongozwa na aliyekuwa msimamizi wa mirathi,Sophia Okashi, Timothy Ndihuri, Willy Mmari walisema kinachofanywa na Halmashauri hiyo, ni kudharau amri halali za mahakama na kutaka kuleta machafuko katika kijiji chao kwani wanajua kesi ilikwisha mahakamani na nyingine zinaendelea.
Okashi alisema, familia yake,ilishinda kesi ya ardhi namba 35/2012 ya kumiliki ardhi yao zaidi ya hekari 2000 ambazo zilikuwa zimevamiwa na wananchi 83 na wakati wa kesi ikiendelea halmashauri walikuwa sehemu ya mashahidi ya waliovamia kesi na hoja ambazo sasa zinaletwa na halmashauri ni zile zile zilizoshindwa mahakamani.
"Sisi tunaomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati kutusaidia ,sisi ni watoto wa marehemu kwa miaka zaidi ya 14 tumehangaika na kesi hii na tumeshinda hadi kugawana mirathi mahakamani na mirathi ikafungwa kisheria sasa leo halmashauri imeibuka tena na kutaka kupora ardhi yetu"alisema
![]() |
Kwa upande wake,Timothy Ndihuri alisema halmashauri ina nia ovu ya kutaka kupora ardhi kwani wanajua washindwa mahakamani na sasa wanatumia nguvu kutaka kupora ardhi ya wananchi.
Marehemu Ahmedi Okashi ambaye alikuwa diwani wa kwanza katika eneoi hili na Baba yangu, walikuwa katika ardhi hii zaidi ya miaka 85 iliyopita na hapa walikuwa wanalima na kuna kila aina ya ushahidi sasa leo halmashauri inakuja na hoja kuwa ardhi hii ni yao ni jambo la aibu sana.
Willy Mmari alisema, ameshangazwa na ardhi yao zaidi ya hekali 1000 kuvamiwa na halmashauri na kuwekewa Bicon bila hata kuwashirikisha wakati kuna kesi inaendelea mahakamani.
![]() |
"Sisi hii ni ardhi yetu na kwa zaidi ya miaka 10 halmashauri imekuwa na mbinu ya kutaka kupora ardhi ili kuuza na kujipatia fedha na ndio sababu tunaomba Rais kuingilia kati kwani hawa ndio wanaigombanisha serikali ya Rais Samia na Wananchi"alisema
Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Jonathan Kiama hata hivyo, alidai wanapima eneo ambalo halina kesi hata hivyo baada ya kupewa ushahidi wa kupimwa eneo lote alisema hukumu ya mahakama kuu haikuainisha mipaka.
Hata hivyo Wakili wa Familia ya Okash, Wakili Gwemelo alipinga hoja za mwanasheria huyo wa halmashauri na kueleza mipaka ilianishiwa kwenye hukumu na hata katika ukazaji wa hukumu ambao tayari ulipitishwa na mahakama.
Hadi kufikia jana bado halmashauri ilikuwa ikiendelea kupima eneo hilo huku maafisa hao, wakiwa wanalindwa na kikosi cha polisi.
Mwisho.






No comments:
Post a Comment