KAMANDA KANTIMBO AFUNGUA MILANGO YA ONGEA NA KAMANDA WA POLISI KWA WANANCHI MOROGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 6 October 2026

KAMANDA KANTIMBO AFUNGUA MILANGO YA ONGEA NA KAMANDA WA POLISI KWA WANANCHI MOROGORO

 

 



Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, ameanza kupeleka Jeshi la Polisi karibu zaidi na wananchi kupitia kampeni ya "Ongea na Kamanda", akisema mapambano dhidi ya uhalifu wa sasa yanahitaji Polisi na jamii kukaa upande mmoja badala ya kila upande kufanya kazi yake pekee.


Kampeni hiyo imezinduliwa katika Kituo kikuu cha Mabasi cha a Msamvu, Morogoro, na kugeuza eneo hilo kuwa jukwaa ambalo wananchi wameweza kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa Polisi kuhusu usalama, changamoto wanazokutana nazo na namna wanavyotaka Jeshi hilo lifanye kazi nao.


Kantimbo alisema Jeshi la Polisi limeona umuhimu wa kubadili namna ya kukabiliana na uhalifu kutokana na mabadiliko ya aina ya makosa yanayotokea, akieleza kuwa wakati uhalifu wa kutumia nguvu ukipungua, wahalifu wanazidi kutumia ujanja, akili, simu na teknolojia kuwafikia wananchi.


Alisema kwa hali hiyo, wananchi hawawezi kubaki watazamaji kwa sababu taarifa wanazokuwa nazo zinaweza kusaidia Polisi kuzuia tukio kabla halijatokea au kuwabaini wahusika baada ya tukio, huku akisisitiza kuwa jukumu la kulinda usalama linahitaji ushiriki wa jamii.


Kantimbo alisema moja ya malengo ya kampeni hiyo ni kuondoa umbali uliopo kati ya Polisi na wananchi kwa kuwasikiliza moja kwa moja, kueleza mambo ambayo huenda wananchi hawayaelewi na kupokea taarifa zinazoweza kusaidia katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Wakazi wa Morogoro

Alisema uwepo wakaguzi wa Polisi ngazi za Kata ni sehemu ya mkakati huo wa kuifanya Polisi iwe karibu na wananchi, huku akiwataka wazazi na walezi kuanzia ndani ya familia kushiriki katika kujenga maadili kwa watoto na vijana, akieleza kuwa mmomonyoko wa maadili unaweza kuwa chanzo cha baadhi ya changamoto za kiuhalifu.


Pamoja na hilo, Kantimbo aliwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha Polisi, huku wale ambao hawahitaji tena silaha walizonazo akiwataka pia kuzifikisha Polisi ili waelekezwe namna salama ya kuzikabidhi.


Katika jukwaa hilo, wananchi hawakuishia kusikiliza, bali wametumia nafasi hiyo kueleza namna wanavyokutana na changamoto za kiusalama ikiwemo ndani na nje ya Kituo cha Mabasi Msamvu, huku baadhi wakieleza kuwa eneo hilo linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Polisi, viongozi wa stendi, wafanyabiashara, waendesha bodaboda na makundi mengine.

Mwananchi akiuliza swali

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni wizi wa mizigo ya abiria, utapeli, watu wanaodaiwa kuingia na silaha au dawa za kulevya na vitendo vya uhalifu vinavyofanyika nyakati za usiku, huku wananchi wakisema watu wanaofanya shughuli mbalimbali katika stendi hiyo pamoja na Kamera zilizopo vinaweza kuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa Polisi.


Mfanyabiashara katika Stendi ya Msamvu, Musa Erasto, amesema wafanyabiashara na watu wengine wanaofanya shughuli zao eneo hilo wana uwezo wa kutambua mienendo ya watu wanaofika na kuondoka, hivyo wanahitaji kuona ushirikiano wao na Polisi ukifanya kazi kwa vitendo.


Erasto amesema hatua ya Polisi kuanzisha jukwaa hilo imeanza kurejesha imani ya wananchi, akieleza kuwa wananchi wako tayari kutoa taarifa na kusaidia Polisi pale wanapoona vitendo vya uhalifu.


Wawakilishi wa waendesha bodaboda na viongozi wa makundi mbalimbali ya stendi nao wamewasilisha hoja zao, zikiwemo namna ya kuhakikisha ukamataji wa watuhumiwa unafanyika kwa kuzingatia usalama na utu, kupambana na rushwa pamoja na kutafuta namna ya kuwawezesha waendesha bodaboda kukamilisha matakwa ya kisheria bila kujikuta wakikwepa Polisi.


Aidha, wananchi walipendekeza matumizi makubwa ya kamera za ulinzi zilizopo katika Stendi ya Msamvu ili kusaidia kufuatilia mienendo ya watu na kubaini matukio yanapotokea, huku viongozi wa makundi mbalimbali wakihimizwa kushiriki kikamilifu katika kuzuia uhalifu.


Kampeni hiyo imekuwa pia jukwaa la Polisi kutoa tahadhari kuhusu aina mpya za uhalifu zinazowafikia wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii.


Mkaguzi wa Polisi, Blastus Lihawa, amewataka wananchi kutomwamini mtu anayewapigia simu na kujitambulisha kuwa mtumishi wa kampuni ya simu au taasisi nyingine bila kwanza kuthibitisha utambulisho wake, huku akisisitiza kutotoa taarifa za siri za akaunti au kufuata maelekezo yanayotolewa na watu wasiojulikana.


Alionya pia dhidi ya tabia ya kutumia taarifa binafsi kusajili laini za simu kwa ajili ya watu wengine na kufungua viungo vinavyotumwa bila kujua vinatoka wapi, akisema hatua hizo zinaweza kumuweka mwananchi katika hatari ya kuhusishwa na uhalifu au kupoteza taarifa na fedha zake.


Kwa upande mwingine, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Uchunguzi Jinai, Kitengo cha Forensic Mkoa wa Morogoro, Martha Abel, alisema mapambano dhidi ya uhalifu hayaishii katika kuwakamata watuhumiwa, bali ushahidi wa kisayansi una nafasi muhimu katika kufuatilia ukweli wa tukio.


Alisema wataalamu wa Forensic hukusanya na kuchambua vielelezo kama alama za vidole, alama nyingine za eneo la tukio, silaha, risasi, nyaraka na vielelezo vingine vinavyoweza kusaidia uchunguzi, huku akiwataka wananchi kutoharibu eneo la tukio kwa kugusa au kuhamisha vitu kabla wataalamu hawajafika.


Kampeni ya Ongea na Kamanda inatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro, huku Jeshi la Polisi likilenga kutumia majukwaa hayo kusikiliza wananchi, kutoa elimu ya kuzuia uhalifu na kujenga ushirikiano wa karibu zaidi na jamii.


Mwisho.

No comments: