Na: Mwandishi wetu - New York.
maipacarusha20@gmail.com
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeelezea mafanikio ya wanawake katika sekta ya uhifadhi na utalii kupitia ushiriki wake katika Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani (CSW69) uliofanyika jijini New York, Marekani kuanzia tarehe 10 hadi 21 Machi, 2025.
Mkutano huu wa Kimataifa, ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa kupitia “UN Women” uliwakutanisha viongozi mbalimbali wa kimataifa kujadili maendeleo ya wanawake duniani.
Katika mkutano huo, TANAPA iliwakilishwa na wanawake viongozi waandamizi na wabobezi katika sekta ya uhifadhi na utalii ambao ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Dkt.Noelia Myonga , Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, CPA. Moureen Mwaimale, Afisa Uhifadhi Mkuu, Bertiller Massawe na Askari Uhifadhi Mkuu Upendo Msaki.
TANAPA iliandaa mkutano wenye mada “Uvunjaji wa Vikwazo: Wanawake,Uongozi na Ujasiriamali katika Sekta ya Utalii Tanzania.” Masuala muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwawezesha wanawake hasa kwenye sekta ya utalii. Pia, TANAPA ilitanabaisha mafanikio yake katika kuendeleza uhifadhi, kukuza utalii na kuongeza mapato kupitia jitihada hizo.
Aidha, Wanawake hao walipata fursa ya kueleza mchango wa Rais Samia katika kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu za “Tanzania: The Royal Tour” na “Amazing Tanzania,” ambazo zimechangia ongezeko la watalii na wawekezaji.
Akizungumza katika Mkutano huo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Dkt.Noelia Myonga alieleza kuwa kutokana na mchango wa wanawake katika uhifadhi na utalii umepelekea kuingiza Hifadhi za Taifa 10 katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za “World Travel Awards 2025” katika vipengele nane. Hifadhi hizo ni Serengeti,Kilimanjaro,Tarangire, Nyerere,Kitulo,Arusha,Katavi,Milima ya Mahale,Milima ya Udzungwa na Ruaha hivyo, nawahamasisha wote tuzipigie kura ili ziweze kushida tuzo hizo”.
Mkutano huo ulifunguliwa na Balozi Gertrude Mongella, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa nne (4) wa Dunia wa Wanawake uliofanyika mwaka 1995, Beijing China.
Ushiriki wa TANAPA katika mkutano huo wa kimataifa ilikuwa ni kujadili masuala mbalimbali kuhusiana na usawa wa kijinsia, mahusiano ya Kimataifa, diplomasia na kukuza uelewa kuhusu haki za wanawake na ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa na Dunia kwa ujumla huku ukionyesha hatua ambazo Tanzania inachukua kuhakikisha wanawake wanashiriki katika uongozi wa sekta ya utalii na uhifadhi.
Mkutano huo ulifungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Zanzibar, Bi. Abeida Rashid kwa kuwataka Wajumbe kuendelea kushiriki katika mijadala mbalimbali inayohusu nafasi ya wanawake katika uongozi, uhifadhi na maendeleo ya sekta ya utalii nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment