BEGA KWA BEGA WAZINDUA HAMASA UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 1 April 2025

BEGA KWA BEGA WAZINDUA HAMASA UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU

 





Na Julieth Mkireri , MAIPAC KIBAHA 


maipacarusha20@gmail.com 


TAASISI ya Bega kwa bega Mkoani Pwani wamefanya bonanza la siku moja kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi mbio za Mwenge wa Uhuru.


Mbio za Mwenge wa Uhuru zinatarajiwa kuzinduliwa kesho April 2 na Makamu wa Rais Dk Philip Isdor Mpango katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.


Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Kibaha Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya Bega kwa bega Ruth Mateleka amesema kazi wanazofanya katika Taasisi yao ni pamoja na kuisemea miradi iliyotekelezwa na Serikali.


Ruth amesema Taasisi hiyo tayari imefika katika mikoa 12 hapa nchini na wameendelea kuizisemea kazi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita Ili wananchi watambue miradi iliyotekelezwa na namna ilivyoondoa kero kwa wananchi.


Mratibu wa Mkoa wa Pwani Zuhura Sekelela amesema bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo ya kuvuta kamba, kutembea na gunia, kukimbiza kuku, mpira wa miguu na ngoma.


"Bonanza letu limelenga kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa ambao unafanyika kesho na sisi tuko tayari kushiriki ," amesema.


Zuhura amesema kwa mkoa huo wamekuwa wakitangaza kazi zilizofanywa na Serikali pia wamekuwa wakifanya usafi wa Mazingira sambamba na kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ikiwemo shule na Hospitali," amesema.


Balozi wa Taasisi hiyo Happiness Ruta amesema pamoja na kishiriki bonanza hilo pia kulikuwa na uchangiaji damu ambao umesaidia kupatikana kwa chupa 19 za damu.


Mchungaji Levalent Mwasulama ambaye ni moja ya washiriki wa bonanza hilo amesema amejiunga na Taasisi hiyo baada ya kuona shughuli wanazofanya ikiwemo kutangaza miradi ya maendeleo.


Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzinduliwa April 2 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha ambapo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema tayari wamefikia asilimia 100 ya maandalizi.


Mwisho

No comments: